Munich, Ujerumani
Bayern Munich imemsimamisha mshambuliaji wake, Sadio Mane anayedaiwa kumpiga ngumi mchezaji mwenzake, Leroy Sane baada ya mechi na Man City huku kukiwa na habari kwamba huenda mchezaji huyo akauzwa.
Katika mechi hiyo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyochezwa Jumanne iliyopita na Bayern kulala kwa mabao 3-0, uliibuka mzozo wa maneno baina ya wachezaji hao uwanjani na baadaye kuendelea kuzozana kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Inadaiwa kwamba baadaye hali ilikuwa tete kiasi cha wachezaji hao kushikana hali iliyowalazimu wachezaji wenzao kufanya kazi ya kuamua ugomvi.
Baada ya tukio hilo, Bayern ilitoa taarifa fupi ya hatua za kinidhamu dhidi ya mchezaji huyo wa zamani wa Liverpool ambaye pia ni mchezaji tegemeo wa timu ya Taifa ya Senegal.
“Sadio Mane, 31, hatokuwa katika kikosi cha Bayern kitakachoumana na 1899 Hoffenheim Jumamosi na sababu ni utovu wa nidhamu wa mchezaji huyo baada ya mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Man City, na zaidi ya hilo atatozwa faini.” ilieleza taarifa ya Bayern kuhusu Mane.
Habari zaidi zinadai kwamba Mane (pchani kushoto) alichukizwa na kauli alizotolewa na Sane baada ya timu hiyo kupokea kichapo cha mabao 3-0 mbele ya Man City kwenye dimba la Etihad.
Bayern haijatoa taarifa nyingine yoyote kuhusu tukio hilo huku ikidaiwa kocha wa timu hiyo, Thomas Tuchel leo Ijumaa huenda akazungumza na waandshi wa habari na kuligusia suala hilo.
Kipigo cha mabao 3-0 ni kikubwa mno kwa Bayern, mara ya mwisho kupata kipigo kama hicho ilikuwa mwaka 2017 mbele ya PSG.
Bayern inajiandaa kurudiana na Man City Aprili 19 mwaka huu katika mechi ambayo itahitaji kupata ushindi wa zaidi ya mabao 3-0 ili kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali.
