Na mwandishi wetu
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Pindi Chana ameipongeza timu ya wasichana ya Fountain Gate kwa kutwaa ubingwa wa Afrika kwa shule za sekondari na kuahidi kukipa kikosi hicho Sh milioni 10.
Pongezi hizo amezitoa Dar es Salaam leo Jumanne katika hafla fupi ya kuwapongeza ambapo pia timu hiyo ilionesha makombe manne iliyotwaa kwenye mashindano hayo ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Makombe hayo ni lile la ubingwa wa Afrika, vikombe vitatu vya mchezaji bora, mfungaji bora na golikipa bora na hundi ya fedha walizotwaa ya Sh milioni 697.
Chana aliupongeza uongozi wa Fountain Gate kwa kuendelea kuthibitisha ubora wa benchi lao la ufundi kwa kufanya maandalizi sahihi ya timu na kupelekea kupata matokeo chanya.
“Nakumbuka mara ya mwisho mliniahidi kutwaa ubingwa wa CECAFA tulipokutana Chamazi katika mashindano ya ukanda wetu wa nchi za Afrika Mashariki na Kati, na kweli mkatwaa ubingwa huo, mara ya pili tulipokutana Machi 31, 2023 mkaniahidi kutwaa Ubingwa wa Afrika mkatekeleza ahadi yenu,”alisema.
Kwa mujibu wa Chana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amewaalika mabingwa hao bungeni Alhamisi hii ili kwenda kupongezwa kwa juhudi walizozifanya.
Kwa upande wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia alisema Fountain Gate imepata jumla ya Dola za Kimarekani 400,000 (zaidi ya Sh milioni 900) ambazo zitatumika kujenga miundombinu ya shule au maabara au hostel.
Alisema kati ya fedha hizo kiasi cha dola 100,000 (Sh milioni 234) ni baada ya kushinda ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) na 300,000 (Sh milioni 697) walishinda kwenye michuno hiyo ya Afrika.
“Uongozi wa Fountain Gate unachotakiwa utengeneze mapendekezo ya matumizi ya fedha hizo zote, nilikuwa naomba mheshimiwa Waziri kama ukihangaika huko uwaongezee kidogo ili wafikishe bilioni moja,” alisema.
Naye mkurugenzi wa shule hiyo, Japhet Makau aliahidi kuendelea kuibua na kuendeleza vipaji vingi kupitia shule hiyo ambayo imekua ikitoka vijana wengi wanaoshiriki katika mashindano mbalimbali ya soka kwa wanawake na wanaume.
“Tuna furaha sababu kazi uliyotutuma tumeitekeleza, ilikuwa ni jukumu zito mbele ya vigogo lakini ulitutia moyo,” alisema.
Soka Pindi Chana aipongeza Fountain Gate
Pindi Chana aipongeza Fountain Gate
Read also
