Munich, Ujerumani
Hofu ya mechi dhidi ya Man City inamtesa kocha wa Bayern Munich, Thomas Tuchel ambaye amekiri mechi hiyo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya inayochezwa leo Jumanne inamnyima usingizi.
Tuchel ambaye anarudi England kwa mara ya kwanza tangu atimuliwe Chelsea Septemba mwaka jana bado ana kumbukumbu jinsi timu hiyo ilivyokuwa ikimpa tabu wakati akiwa kocha Chelsea.
Katika mechi 10 ambazo amekutana na Man City wakati akiwa kocha wa Chelsea, Tuchel ameshinda mara tatu tu.
Akiizungumzia mechi hiyo jana Jumatatu na jinsi inavyomnyima usingizi, Tuchel alisema, “Nitajaribu kwenda kulala mapema, natumaini nitaweza kupata usiingizi.”
“Maandalizi mazuri ni pamoja na kulala lakini kuna wakati ni vigumu kupata usingizi unapokuwa unafikiria mambo,” alisema Tuchel.
“Asubuhi hii (jana Jumatatu) niliamka mapema na nikaamua kwenda mazoezini kwa sababu sikuweza kupata usingizi, kitu pekee nilichokuwa nakifikiria mara kwa mara ni hii mechi,” aliongeza Tuchel.
Tuchel akiwa Chelsea aliifunga Man City chini ya Pep Guardiola mara ya mwisho mwaka 2021, timu hizo zilipokutana kwenye mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Tuchel kubeba taji lake la kwanza kati ya matatu aliyoyabeba akiwa Chelsea.
Tuchel ambaye alikabidhiwa mikoba ya kuinoa Bayern mwezi uliopita akichukua nafasi ya Julian Nagelsmann aliyetimuliwa, alisema kwamba timu yake inatakiwa kuutawala mchezo ili kuishinda City ambayo imekuwa na rekodi nzuri katika mechi zake nane zilizopita.
“Sidhani kama naweza kujifunza mengi katika mechi nyingine za City chini ya Pep, anayofanya Pep ni mambo ya kipekee, tutajaribu kutafuta suluhisho lakini tunahitaji kiwango bora ili kuwaweka City katika matatizo,” alisema.
Mechi za robo fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya Leo Jumanne
Man City v Bayern Munich, saa 4:00 usiku
Benfica v Inter Milan, saa 4:00 usiku
Mechi za robo fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya kesho Jumatano
AC Milan v Napoli, saa 4:00 usiku
Real Madrid v Chelsea, saa 4:00 usiku
