Na mwandishi wetu
Bondia Twaha Kassim ‘Kiduku’ amesema anajifua vikali kuhakikisha anaibuka na ushindi dhidi ya mpinzani wake Iago Kiziria raia wa Georgia kwenye pambano lake la Aprili 23, mwaka huu.
Pambano hilo ambalo ni la kwanza kwa Kiduku mwaka huu, litapigwa kwenye Ukumbi wa Tanzanite, Morogoro likiwa limepewa jina la Mfalme Kwenye Ufalme Wake hivyo Kiduku amedhamiria kuonesha ufalme wake siku hiyo.
“Namshukuru Mungu kwa nilipofikia kwenye kujiandaa kuitetea nchi yangu dhidi ya bondia Iago, tuko kwenye maandalizi makubwa na mwalimu wangu, naendelea vizuri na nimefurahi hii mechi imeletwa Morogoro, niwaambie mashabiki wangu niko poa na kwa uwezo wa Mungu ushindi utabaki Tanzania,” alisema Kiduku.
Alisema anafahamu hakuna pambano rahisi hasa mpinzani anayekutana naye si mwepesi na amekuwa na rekodi nzuri hivyo anajifua kuhakikisha anapata ushindi mkubwa dhidi ya bondia huyo na kuwafurahisha Watanzania.
“Najua halitokuwa pambano rahisi hata kidogo kutokana na rekodi yake (Iago) lakini nataka kuwaambia mashabiki wangu safari hii nitafanya balaa kubwa. Imekuwa ikiwakera wengi nikishinda kwa pointi na mabondia wote nimekuwa nikiletewa si wepesi hata kidogo ila safari hii K.O itahusika, naomba wajitokeze kwa wingi,” alisema.
