Manchester, England
Kocha wa Man United, Eric ten Hag amesema mambo si mazuri kwa straika wake, Marcus Rashford ingawa amefurahia kiwango cha beki Harry Maguire ambaye kwa muda mrefu amekuwa akisugua benchi.
Rashford aliumia jana Jumamosi wakati timu hiyo ikiichapa Everton mabao 2-0 katika mechi ambayo Ten Hag pia alimpa nafasi nahodha na beki wa kati Maguire ambaye amepoteza namba kikosi cha kwanza.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu England (EPL), Rashford alipata matatizo ya misuli muda mfupi kabla ya filimbi ya kumaliza mchezo huo kupulizwa na baadaye alionekana akitoka uwanjani katika hali ya unyonge.
Na ingawa Ten Hag awali alipoulizwa kuhusu mchezaji huyo na ukubwa wa maumivu aliyoyapata alikataa kuzungumzia hilo kwa undani na kuhoji wenye hofu hiyo kama wao ni madaktari.
Kocha huyo hata hivyo alilalamikia ugumu wa ratiba inayoikabili timu hiyo na kusema kuwa mambo si mazuri kwa mchezaji huyo na kuhusisha ratiba hiyo ngumu na maumivu ya mchezaji huyo.
“Tunalazimika kusubiri hali haionekani kuwa nzuri, hali hii inaweza kuepukwa, sayansi na tafiti zote zinasema wachezaji wanahitaji muda kwa ajili ya kupumzika na kujiweka sawa,” alisema Ten Hag.
“Hii inachangiwa na ratiba tuliyonayo hadi tunajikuta katika mazingira ya aina hii na sasa tunachoweza kufanya ni kuomba asiwe wa kutolewa kwenye kikosi moja kwa moja,” alisema.
Ten Hag pia alikiri kwamba angeweza kumtoa Rashford baada ya United kupata bao la pili dakika ya 19 lakini hakuwa tayari kufanya hivyo kwa sababu alitaka mfungaji wake huyo bora apate muda wa kucheza pamoja na Anthony Martial aliyerejea.
“Sidhani kama kuna kocha yeyote katika kipindi hiki cha msimu anaweza kubadili badili wachezaji wake kwa sana, nilikuwa na fikra hizo za kumtoa nje lakini kwa kipindi hiki ndio kwanza Anthony Martial amerejea unataka wawe pamoja,” alisema.
“Wanapokuwa pamoja hapo tunakuwa na wafungaji wawili ambao wanaweza kumaliza mechi kitu ambacho tunakihitaji katika hatua hizi za mwisho za msimu ili kuwa na mafanikio,” aliongeza Ten Hag.
Kuhusu Maguire, Ten Hag pia alieleza kufurahishwa na kiwango cha nahodha huyo akisema kwamba hapo kabla hakumuona akicheza kwa ubora huo.
“Huyu alikuwa Harry Maguire mwingine kabisa, tofauti na yule wa wiki au miezi ya mwanzo, mambo hayakuwa rahisi kwake lakini ni yeye aliyekuwa akitaka kucheza na alicheza vizuri mno leo (jana) awe na mpira au asiwe na mpira, aliwadhibiti wapinzani wake, aliongoza mchezo na kutoa pasi,” alisema Ten Hag.
Maguire beki aliyesajiliwa kwa Pauni 80 milioni amekuwa na wakati mgumu kupata namba katika kikosi cha kwanza cha Man United kwa kilichoonekana kuwa ni kushuka kiwango lakini Ten Hag ameendelea kumuamini katika nafasi ya nahodha wa timu.
