Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele amesema ushirikiano wake na Kennedy Musonda unazidi kuimarika akieleza uwepo wa mchezaji huyo utawasaidia mno kwenye mashindano ya klabu Afrika.
Mayele ambaye anaongoza kwa kufunga mabao 15 kwenye Ligi Kuu NBC amesema mashabiki na wadau wa soka wategemee mazuri kutoka kwa wawili hao.
“Nadhani wategemee mazuri zaidi, tutaendelea kupambana kwa pamoja, sisi wote tunategemeana na nadhani (Musonda) amekuja kuongeza kikubwa kwenye timu na anatusaidia sana, sana mechi za kimataifa na hatutaishia hapa,” alisema Mayele.
Musonda (pichani) aliyetua kwenye dirisha dogo la usajili msimu huu akitokea Power Dynamos ya kwao Zambia amekuwa na ushirikiano mkubwa kwa kutoa pasi za mabao na kufunga katika mechi za hivi karibuni.
Mayele pia alieleza kufurahia kukutana kwa mara nyingine na Rivers United katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika akijinadi kuwa huu ndiyo wakati sahihi kwao kulipa kisasi kwa timu hiyo ya Nigeria.
“Tumempata mpinzani ambaye kila mmoja alikuwa anamtamani, binafsi nilikuwa namtaka nadhani mwaka jana hatukucheza naye tukatolewa mapema watu wakaongea sana na sasa tumempata sehemu nzuri kwa hiyo tutaenda mazoezini kufanya kazi ya kujiandaa, tutalipa kisasi,” alisema Mayele.
Yanga iliondoshwa na Rivers kwenye mechi za kuwania kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2021/22 kwa kufungwa mechi ya kwanza nyumbani bao 1-0 kabla ya kukutana na kipigo kama hicho katika mechi ya marudiano ugenini.
Mchezo wa kwanza wa robo fainali baina ya timu hizo, utapigwa Apirli 23 nchini Nigeria kabla ya mechi ya marudiano itakayochezwa Aprili 30, mwaka huu.