Na mwandishi wetu
Simba imetua nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Azam (ASFC) baada ya kuitia adabu Ihefu FC kwa kuichapa mabao 5-1 huku straika wake Jean Baleke akifunga mabao matatu kati ya hayo.
Ihefu timu iliyovuruga rekodi ya Yanga iliyokuwa ikiwania kucheza mechi 50 bila kupoteza hata moja, ilikutana na kipigo hicho Ijumaa hii usiku kwenye dimba la Azam Complex na kuaga michuano hiyo.
Kwa ushindi huo Simba sasa inasubiri kuivaa Azam katika hatua ya nusu fainali wakati Yanga ikiisaka tiketi ya nusu fainali kwa kuivaa Geita Gold Jumamosi usiku.
Nyota ya Baleke katika mchezo huo ilianza kung’ara katika dakika ya tatu baada ya kuandika bao la kwanza kabla ya kufunga mabao mengine mawili katika dakika za 17 na 28.
Baleke aliyesajiliwa Simba Januari mwaka huu wakati wa dirisha dogo sasa amefikisha jumla ya mabao 12 katika michuano yote aliyoichezea Simba huku matano kati ya hayo yakiwa ya Ligi Kuu NBC.
Zikiwa zimebakia dakika tano timu kwenda mapumziko, Simba iliandika bao la nne lililofungwa na Saido Ntibazonkiza, nyota mwingine aliyesajiliwa Simba katika dirisha dogo akitokea Geita Gold.
Mabao hayo hayakuwakatisha tamaa Ihefu ambao walipambana na kupata bao lao pekee katika mchezo huo lililofungwa na Raphael Daud katika dakika ya 61.
Zikiwa zimebakia sekunde chache kabla ya mwamuzi kupuliza filimbi ya kumaliza mchezo, mambo yalizidi kuwaharibikia Ihefu walipojikuta wakipachikwa bao la tano lililofungwa na Pape Sakho.
Soka Simba yaitia adabu Ihefu
Simba yaitia adabu Ihefu
Read also
