Cairo, Misri
Yanga itaanza kuisaka tiketi ya nusu fainali Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuivaa Rivers United ya Nigeria wakati Simba wataanza kuisaka tiketi hiyo katika Ligi ya Mabingwa kwa kuumana na Waydad Casablanca ya Morocco.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya droo iliyofanyika Jumatano hii usiku na sasa wawakilishi hao pekee wa Tanzania na Afrika Mashariki wataanza kupigania tiketi hiyo kati ya Aprili 23 ambapo Yanga itaanzia ugenini na kurudiana Aprili 30 jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa Ligi ya Mabingwa kazi itaanza kati ya Aprili 21 au 22 ambapo Simba itaanzia jijini Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana wiki moja baadaye katika jiji la Casablanca nchini Morocco.
Yanga bado inakumbukumbu mbaya ya Rivers ambapo mara ya mwisho timu hizo zilikutana mwaka 2021 kwenye Ligi ya Mabingwa ambapo Yanga ilipoteza mechi zote mbili.
Katika mechi ya kwanza nyumbani Yanga ililala kwa bao 1-0 kabla ya kukutana na kipigo kama hicho katika mechi ya marudiano ugenini mjini Portha.
Kwa hali hiyo, Yanga ni kama vile imepata nafasi ya kulipa kisasi dhidi ya timu ambayo iliwatoa kwenye mashindano hayo ya Afrika mwaka 2021.

Nusu fainali za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho zote zitachezwa kati ya Mei 14 na 21 na baada ya hapo washindi wataumana katika hatua ya fainali kati ya Juni 4 na 11 kwa mtindo wa nyumbani na ugenini.
Mechi za robo fainali Ligi ya Mabingwa ni kama ifuatavyo…
Simba vs Wydad Athletic
Al Ahly vs Raja Casablanca
CR Belouizdad vs Mamelodi Sundowns
Kabylie vs Esperance
Mechi za robo fainali Kombe la Shirikisho ni kama ifuatavyo…
Pyramids v Marumo Gallants
US Monastir v ASEC Mimosas
USM Alger v FAR Rabat
Rivers Utd v Yanga