Na mwandishi wetu
Baada ya Simba na Yanga kuwafahamu wapinzani wao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, makocha wa timu hizo wamesema wana nafasi ya kufanya vizuri.
Katika droo iliyochezeshwa Cairo, Misri Jumatano hii usiku na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), Simba ilipangwa kukutana na bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa, Wydad Casablanca ya Morocco kwenye hatua ya robo fainali huku Yanga ikiangukia kwa Rivers United ya Nigeria.
Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema kuwa katika hatua hiyo hakuna timu rahisi ila hana wasiwasi na wapinzani wake kutokana na uimara wa kikosi chake.
“Kwenye hatua hii ya Ligi ya Mabingwa hakuna mechi rahisi lakini nina uhakika nitafanya vizuri kutokana na wachezaji nilionao wenye uzoefu na kikosi imara. Nafurahi namna walivyocheza vizuri na kwa muunganiko katika michezo iliyopita,” alisema Robertinho.
Hii ni mara ya tatu katika misimu miwili Simba kukutana na timu za Morocco ambapo katika hatua ya makundi ilikutana na Raja Casablanca na msimu uliopita walicheza na RS Berkane kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze alisema: “Kikubwa sisi wenyewe tunaamini kwamba uwezo wetu ni mkubwa na mzuri na ndio maana tunaamini kuna nafasi pale ya kufanya kazi na kuingia hatua ya nusu fainali.
“Timu zote zilizoingia hatua ya robo fainali ni nzuri, zimejiandaa na zimefanya vizuri hadi kufika hapo hivyo tunapaswa kujipanga vizuri kuwa imara na tayari kwa mapambano,” alisema Kaze.
Mara ya mwisho walikutana katika mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa mwaka juzi na Yanga kupoteza michezo yote miwili, ikifungwa kila mmoja bao 1-0.
Yanga itaanzia ugenini Aprili 23 kisha itacheza mchezo wa marudiano nyumbani Aprili 30, mwaka huu wakati Simba itavaana na Wydad ikiwa nyumbani Aprili 21 kabla ya mchezo wa marejeano Aprili 28, mwaka huu.

Endapo Simba itamtoa Wydad itakutana na mshindi kati ya CR Belouzidad ya Algeria na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika nusu fainali wakati Yanga itakutana na mshindi wa mechi kati ya Pyramids ya Misri na Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
