Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele amesema kwa sasa wanajiandaa vilivyo kwa ajili ya mechi tatu alizotafsiri ni ngumu lakini wanataka kuhakikisha wanashinda zote.
Mayele alizitaja mechi ngumu mbele yao kuwa ni ile ya robo fainali ya Kombe la FA (ASFC) dhidi ya Geita Gold itakayochezwa Jumamosi hii, mechi mbili za Ligi Kuu NBC dhidi ya Kagera Sugar na Simba.
“Tumemaliza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika salama na tunashukuru Mungu kwamba tunaongoza na sasa malengo yetu tunatazama michezo mitatu migumu iliyoko mbele yetu, tunahitaji kujipanga kujiweka imara kwa michezo hiyo,” alisema Mayele.
Mchezaji huyo anayeongoza katika orodha ya wafungaji bora kwa kufunga mabao 15 kwenye ligi alisema anaamini wakifanya maandalizi mazuri kwa kila mchezo wana nafasi ya kuendeleza ubora wao.
Wachezaji wa Yanga baada ya kurejea Dar es Salaam wakitokea DR Congo wameelekea kambini kujiandaa na michezo hiyo yenye umuhimu wa kuamua hatma yao ya utetezi wa mataji waliyonayo.
Yanga ndiye bingwa mtetezi wa kombe la FA na ligi kuu na wamedhamiria kuendelea kufanya vizuri kuyatetea kwa msimu wa pili mfululizo.
Yanga inaongoza msimamo wa ligi ingawa hawawezi kujihakikishia nafasi ya kuchukua taji hadi washinde michezo minne ijayo.
Katika michezo 24 waliyocheza, Yanga wameshinda 17, sare sita na kupoteza mchezo mmoja wakiwa na pointi 65. Tofauti ya pointi nane dhidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili.
