London, England
Leicester City imeachana na kocha Brendan Rodgers baada ya timu hiyo kufungwa mabao 2-1 na Crystal Palace juzi Jumamosi na tayari bodi imeahidi kuchukua hatua kuhakikisha timu haishuki daraja.
Rodgers aliyekabidhiwa jukumu la kuinoa timu hiyo Februari 2019, Jumamosi aliishuhudia ikikutana na kipigo cha sita mfululizo katika Ligi Kuu England na hivyo kujiweka katika hatari ya kushuka daraja.
Mwenyekiti na mmiliki wa klabu hiyo, Aiyawatt Srivaddhanaprabha alisema kwamba kiwango cha timu na matokeo yamekuwa chini ya matarajio.
“Ni imani yetu kwamba mazingira endelevu na uimara yote hayo yatakuwa msingi wa kurekebisha hali tuliyonayo hasa tukizingatia mafanikio yetu yaliyopita chini ya Brendan,” ilieleza taarifa ya klabu hiyo ikimtaja kocha huyo ambaye mwaka 2021 aliiwezesha timu hiyo kutwaa taji la FA.
“Katika hali ya kusikitisha matarajio ya kuboresha timu hayakufikiwa na zikiwa zimebaki mechi 10 kumaliza msimu bodi imelazimika kuchukua hatua zinazowezekana ili kulinda hadhi yetu katika ligi kuu,” ilifafanua taarifa ya klabu hiyo.
“Jukumu lililo mbele yetu katika mechi 10 za mwisho lipo wazi, sasa tunahitaji kuwa pamoja, mashabiki, wachezaji na maofisa wa timu na kupigania nafasi yetu katika ligi kuu.”
