Na mwandishi wetu
Yanga imeimarisha nia yake ya kutaka kumaliza mechi za Kundi D za Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa kinara wa kundi hilo baada ya kuilaza TP Mazembe bao 1-0 katika mechi iliyopigwa mjini Lubumbashi.
Kwa ushindi huo uliopatikana leo Jumapili, Yanga sasa imefikisha pointi 13 ikiwa kinara wa kundi hilo ikifuatiwa na US Monastir ya Tunisia inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 10.
Kinachoweza kuikwamisha Yanga kumaliza mechi za kundi hilo ikiwa kinara ni mechi kati ya Monastir na Real Bamako ya Mali itakayopigwa baadaye leo usiku.
Monastir italazimika kupata ushindi wa zaidi ya mabao mawili ili kufikisha pointi 13 na kuipiku Yanga kwa tofauti ya mabao ya kufunga ambayo ndiyo yanayoifanya Yanga ishike usukani wa kundi hilo.
Katika mechi ya leo aliyeipa Yanga bao pekee alikuwa ni Farid Mussa katika dakika ya 64 alipoujaza mpira wavuni kwa shuti kali baada ya kipa wa Mazembe kuokoa krosi iliyochongwa na Moloko.
Huu unakuwa ushindi wa pili kwa Yanga dhidi ya Mazembe baada ya kuichapa timu hiyo mabao 3-1 katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mazembe nao walilisakama mara kadhaa lango la Yanga lakini safu ya ulinzi ya timu hiyo ikiwa na mlinda mlango Beno Kakolanya ilikuwa mkini kudhibiti mashambulizi hayo.
Yanga na Monastir tayari zimefuzu hatua ya robo fainali zikisubiri Aprili 5 kuwajua wapinzani wao katika hatua hiyo wakati Real Bamako na Mazembe zimeaga rasmi michuano hiyo katika hatua ya makundi.
Kimataifa Yanga yaipiga Mazembe Lubumbashi
Yanga yaipiga Mazembe Lubumbashi
Read also
