Na mwandishi wetu
Kocha wa zamani wa Yanga Princess, Edna Lema (pichani) amesema kuwa anaamini atakuwa kocha wa kwanza mwanamke kuinoa timu ya Ligi Kuu NBC kwa kuwa anaamini ana uwezo wa kufanya hivyo.
Edna maarufu kwa jina la Mourinho ameyasema hayo baada ya juzi kutambulishwa kuinoa timu ya wanaume ya Mkwabi FC inayoshiriki michuano ya Kombe la Ramadhan inayoendelea jijini Dar es Salaam.
Alisema ni muda mrefu amekuwa akitamani kuinoa timu ya wanaume bila ya kujali ni mashindano gani baada ya kukaa kwenye soka la wanawake kwa muda mrefu lakini sasa anaamini pia iko siku atatimiza ndoto yake ya kutua ligi kuu.
“Mimi nafikiri katika kazi ya ukocha ni kuishi na kujifunza, yawezekana kila kitu mwanzo ni kigumu lakini unaweza kuona ugumu sababu uko nje, ukiwa ndani utaona sababu hata kwa wanawake kuna ugumu pia lakini kwangu mimi nimeona hata kufundisha wa kiume ni rahisi.
“Natamani kuona siku moja na ninaamini nitakuwa kocha wa kwanza mwanamke kufundisha timu ya wanaume, kwangu natamani hata kesho nipate timu ya Ligi Kuu Tanzania, niwe kocha msaidizi au kocha mkuu naamini uwezo ninao, sitaki kujiweka kwenye nafasi ya siwezi,” alisema Edna.
Alisema kuwa anaamini kila kitu ni kujifunza na hata timu anayoinoa sasa imempa mwanga kwa namna wanaume wanavyoitikia na kusikiliza mafunzo yake na hata namna anavyowasiliana nao kumekuwa na utofauti na namna alivyokuwa akifikiria mwanzo kuwa kutakuwa na ugumu.
Edna aliachana na Yanga mwanzoni mwa msimu huu na mikoba yake kukabidhiwa Sebastian Nkoma kabla naye juzi kuondolewa katika kiti hicho na nafasi yake inakaimiwa na Fred Mbuna, mchezaji wa zamani wa Yanga SC.