Na mwandishi wetu
Beki mpya wa kati wa Yanga, Mamadou Doumbia ameahidi kupambana mazoezini ili kumshawishi kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi ili ampe nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.
Mchezaji huyo raia wa Mali, tangu ametua Yanga akitokea Stade Meliane ya Mali kwenye dirisha dogo la usajili msimu huu ametumika kwa dakika 45 kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyofanyika Zanzibar.
Mchezaji huyo ameeleza kuwa kinachomfanya asipate nafasi tangu ajiunge na timu hiyo ni kufanyia kazi mifumo ya kiuchezaji ambayo wachezaji wenzake tayari wameshaizoea. “Bado kuna vitu havijawa sawa kwangu kama kufuata vizuri mbinu ambazo kocha anataka tucheze lakini vitu vingine vyote ikiwemo namna ya kushirikiana na wenzangu pamoja na kuanzisha mashambulizi nipo sawa,” alisema Doumbia.
Mchezaji huyo ameeleza kuwa pamoja na changamoto hizo lakini hajakata tamaa, ataendelea kupambana kupigania nafasi ya kucheza na anaamini siku chache zijazo ataanza kuitumikia timu hiyo.
Alisema mbali na kuyafanyia kazi maelekezo ya benchi la ufundi lakini pia amekuwa akijifunza kutoka kwa wachzaji wenzake namna ya kutimiza kile ambacho wanatakiwa kukifanya hivyo mashabiki watarajie kumuona uwanjani hivi karibuni.
Doumbia ambaye mashabiki wengi wamekuwa wakitamani kumuona akikipiga kwenye mechi za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika, anapokea ushindani mkubwa kutoka kwa mabeki wa nafasi hiyo aliowakuta, nahodha Bakari Mwamnyeto, Dickson Job, Ibrahim Bacca na wakati mwingine Yanick Bangala.