London, England
Baada ya kumshutumu mmiliki wa klabu ya Tottenham Hotspur na wachezaji wa timu hiyo akidai ni wabinafsi, hatimaye kocha Antonio Conte ametangaza kung’atuka kuinoa timu hiyo.
Mara baada ya Conte kuchukua uamuzi huo binafsi jana Jumapili jioni, msaidizi wake, Cristian Stellini amekabidhiwa majukumu ya Conte na Ryan Mason ameteuliwa kuwa msaidizi wa Stellini.
Wiki iliyopita, Conte aliyekuwa kocha wa Spurs kwa miezi 16 iliyopita alimshutumu mwenyekiti na mmiliki wa klabu hiyo, Dany Levy akimshangaa kuimiliki klabu kwa muda mrefu bila mafanikio yoyote.
Kauli hiyo ya Conte ilitafsiriwa kwamba ni ama alijiandaa kwa lolote lakini kwa wengi iliaminika kwamba siku zake katika klabu hiyo zilikuwa zikihesabika.
Spurs kwa sasa inashika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu England (EPL) na matumaini ya kubeba taji lolote msimu huu yakizidi kuyeyuka baada ya kutolewa katika mshindano mengine jambo lililosababisha kuyumba kwa uhusiano kati ya Conte na mabosi wake.
Akizungumza mara baada ya Conte kutangaza kuondoka katika klabu hiyo, Levy alisema, “Tuna mechi 10 za ligi kuu zimebaki na tuna vita ya kupigania kusaka nafasi ya kushiriki ligi ya mabingwa.”
“Sote tunahitaji kuweka mambo yetu pamoja, kila mmoja anatakiwa kujiweka sawa kuhakikisha tunamaliza tukiwa juu kadri iwezekanavyo kwa ajili ya klabu yetu na mashabiki wetu,” alisema Levy.
