Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema timu yake bado ina nafasi ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu NBC licha ya kuzidiwa kwa pointi nane na vinara wa ligi hiyo, Yanga.
Robertinho amesema pamoja na kukabiliwa na kibarua kizito kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, bado hajakata tamaa na ubingwa wa ligi kuu na hiyo ni kutokana na idadi ya michezo iliyobaki kati yao na watani zao Yanga.
“Tutaendelea kuzitumia mechi sita zilizobaki kuwatia presha Yanga ikiwezekana kupunguza idadi ya pointi nane iliyopo hivi sasa na ukizingatia tuna mchezo nao siku chache zijazo,” alisema Robertinho.
Kocha huyo ameeleza kuwa anajua si kazi rahisi kulingana na ubora waliokuwa nao wapinzani wao lakini Simba ina wachezaji wapambanaji wanaofuata kwa weledi mkubwa mbinu anazowapa.
Anaamini kuelekea mchezo wao dhidi ya Yanga utakaopigwa Aprili 16, mwaka huu ni nafasi nzuri pia kuitumia na kupunguza ukubwa wa pengo la pointi baina yao.
Alisema kuiruhusu Yanga, kubeba ubingwa huku wao wakiachwa kwa idadi hiyo ya pointi haileti picha nzuri kwao hivyo kama ikitokea wameshindwa kubeba ubingwa basi kupunguza pengo la pointi angalau zibaki mbili au tatu.
Simba imeingia kambini jana jioni kujiandaa na mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Raja Casablanca, mchezo ambao utapigwa Morocco mwishoni mwa mwezi Machi.
