Barcelona, Hispania
Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa) linaanza uchunguzi wa malipo yanayotiliwa shaka ambayo Barcelona inadaiwa kumlipa makamu rais wa zamani wa kamati ya waamuzi Hispania.
Katika mpango huo tayari shirikisho hilo limeteua wachunguzi wa maadili na nidhamu ili kufanya uchunguzi kuhusu malipo hayo ambayo inadaiwa yalilipwa ili klabu hiyo ipewe upendeleo na waamuzi.
Mahakama moja mjini Barcelona tayari imeshaarifiwa kuhusu tukio hilo linalodhaniwa kuwa ni la utoaji rushwa, kukosekana uaminifu na taarifa zisizo sahihi za kibiashara.
Waendesha mashitaka wa Barcelona walidai kwamba klabu ya Barcelona au Barca ilimlipa makamu huyo wa rais wa zamani, Jose Maria Negreira Pauni 7.4 milioni kupitia kampuni yake ya Dasnil 95.
Barca mbali na kukana kufanya kosa lolote lakini imekiri kutoa malipo ya aina hiyo kwa kampuni ya Dasnil 95 kati ya mwaka 2001 na 2018.
“Wachunguzi wa nidhamu na maadili wameshateuliwa ili kufanya uchunguzi wa kinachodhaniwa kuwa ni klabu ya Barcelona kwenda kinyume na taratibu za Uefa kuhusiana na malipo yanayodaiwa kufanywa kwa anayetajwa kuwa ni Negreira,” ilieleza taarifa ya Uefa.
Kwa upande wa Barca wamedai kuwa kampuni hiyo wanaitumia katika ushauri wa kiufundi na ililipwa ili kuandaa taarifa ya video kuhusu waamuzi ili kupata taarifa ambazo benchi la ufundi ilizihitaji.
Marais wa zamani wa Barca, Josep Maria Bartomeu na Sandro Rosell pamoja na Negreira, wote wamehusishwa katika sakata hilo pamoja na klabu.
Mtendaji Mkuu wa La Liga, Javier Tebas ameahidi kushirikiana na mamlaka kuhusu sakata hilo kama ilivyo kwa klabu ya Real Madrid lakini Tebas amekwenda mbali zaidi akimtaka rais wa sasa wa Barca, Joan Laporta ajiuzulu.
Kimataifa Uefa yajitosa kashfa ya Barca
Uefa yajitosa kashfa ya Barca
Read also
