Naples, Italia
Kocha wa zamani wa Man City, Roberto Mancini amekana kufanya kosa lolote na hatarajii kuhojiwa wakati klabu hiyo ikiandamwa na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha ikiwamo malipo ya mishahara.
Mancini ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya Taifa ya Italia, amesema hatarajii kuwa sehemu ya watu watakaohojiwa katika uchunguzi unaofanywa na tume huru ya Ligi Kuu England (EPL).
Mwezi uliopita Man City ilihusishwa katika tuhuma za makosa zaidi ya 100 ya matumizi ya fedha kati ya mwaka 2009 na 2018 pamoja na klabu hiyo kutotoa ushirikiano katika sakata hilo tangu Desemba 2018.
Mabosi EPL walitaka kujua iwapo Man City iliweka taarifa zote muhimu za mkataba wa Mancini kati ya mwaka 2009 na 2013 wakati akiwa kocha wa timu hiyo na kuwapa taji la kwanza baada ya miaka 44.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari, Mancini inadaiwa kuna wakati alikuwa akilipwa mshahara wa Pauni 1.45 milioni na Pauni 1.75 milioni kama mshauri wa timu na mmiliki wa klabu hiyo, Sheikh Mansour wa Abu Dhabi.
Baadhi ya wachunguzi walitaka jambo hilo lichunguzwe wakiwa wamejenga hisia kwamba huenda kulikuwa na makubaliano ya siri yenye lengo la ‘kucheza’ na mshahara huo ili uonekane mdogo.
Man City imekana kufanya kosa lolote wakati huu ambapo tume huru inajiandaa kufanyia kazi ushahidi wa sakata hilo.
Akizungumza wakati England ikijiandaa kuuman ana Italia mjini Naple leo Alhamisi jioni, Mancini aliulizwa iwapo aliwasiliana na wajumbe wa tume huru na kuhojiwa lakini alisema hajahojiwa kwa lolote.
“Hapana, sijahojiwa au kuitwa kokote na mtu yeyote na sidhani kama kuna mtu amewahi kuwasiliana nami, nimelipa kodi zangu, hayo ni mambo ya bodi kwa hiyo sidhani kama kuna atakayewasiliana na mimi,” alisema Mancini.
