Na mwandishi wetu
Kikosi cha Yanga kinatarajia kuanza mazoezi leo Alhamisi kujiandaa na mchezo wa kuhitimisha hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo (DRC) utakaochezwa Aprili 2, mwaka huu mjini Lubumbashi.
Yanga ndiye kinara wa kundi D baada ya kufikisha pointi 10 sawa na US Monastir ya Tunisia huku Real Bamako ikiwa na pointi tano na Mazembe ya mwisho ikiwa na pointi tatu.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo Dar es Salaam leo Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema wachezaji ambao hawajaitwa kwenye majukumu ya timu za taifa wataanza mazoezi kisha Jumatatu wataingia kambini rasmi kwa maandalizi ya jumla.
“Wachezaji ambao hawamo kwenye timu ya taifa wataanza mazoezi hadi tarehe 27 timu itaingia kambini rasmi, tunataka ushindi katika mchezo ili kuendelea kusalia katika uongozi hivyo lazima timu ijipange vizuri,” alisema Kamwe
Kamwe alisema kuna faida timu ikimaliza katika uongozi kwani michezo ya hatua ya robo fainali wataanzia ugenini kisha watamaliza nyumbani na kwa kulitambua hilo wanaona mchezo ujao ni muhimu kwenda kupambana na kushinda ili kulinda nafasi waliyopo.
Akizungumzia safari ya mashabiki kwenda Lubumbashi kushuhudia mechi hiyo kuwa basi lipo kwa gharama ya Sh 700,000 ambapo ndani ya gharama hizo ni nauli ya kwenda na kurudi, malazi, tiketi na vibali ikiwemo chanjo ya corona na kugongewa mihuri mpakani.
Alisema safari kwa mashabiki itaanza Machi 30, mwaka huu ila timu itasafiri kwa ndege. “Niwaombe mashabiki, fursa imekuja mbele yetu na tunafika DRC tukiwa hatuna presha yoyote. Lakini ni mchezo muhimu kwa klabu yetu na tunatambua thamani ya kumaliza tukiwa kwenye kilele cha msimamo,” alisema.
“Umuhimu wa mchezo huo unahitaji sapoti ya mashabiki kwenda kuishangilia timu ipate matokeo. Haijalishi kwamba tumeshafuzu, tunachotaka ni kushinda na kurudi tukiwa na furaha ya kumaliza tukiwa tunaongoza kundi,” alisema.
