Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Geita Gold, Fredy Minziro ametamba kuwa atapambana kuhakikisha timu yake inakuwa kati ya timu nne zitakazopeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa msimu ujao.
Tanzania itapeleka timu nne kwenye michuano ya klabu Afrika baada ya timu za Simba na Yanga kufanya vizuri kwenye mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika ikiwemo timu zote mbili kutinga hatua ya robo fainali.
Kocha huyo ameeleza kuwa malengo yake ni kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mashindano yote mawili wanayoshiriki kwa maana ya Ligi Kuu NBC na Kombe la FA, ambayo ndio yanatoa nafasi za kushiriki michuano hiyo.
“Tunaitaka michuano ya kimataifa kwa mara nyingine tena baada ya mwaka huu kutolewa hatua ya awali, kitu kizuri nafasi ya kufanya hivyo bado ipo sababu kwenye msimamo wa ligi tupo nafasi ya tano na kwenye Kombe la FA tupo robo fainali na tutacheza na Yanga hilo halitupi presha,” alisema Minziro.
Minziro amesema kuwa wapinzani wao wakubwa katika kampeni ya kusaka nafasi ya kuwakilisha taifa kwenye michuano ya kimataifa ni Azam na Singida Big Stars ambazo zipo juu yao kwenye msimamo wa ligi na imani yake ni kushinda mechi zao tano zilizobaki kwenye ligi ili kupata nafasi hiyo.
Alisema kwenye Kombe la FA, anajua wanakwenda kukutana na bingwa mtetezi Yanga, anajua utakuwa mchezo mgumu lakini wamejipanga kuhakikisha wanapambana kuvuka kigingi hicho ili kuendelea kwenye hatua zinazofuata na kutinga fainali.
Geita msimu huu ilitolewa kwenye hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho na Hilal Alsahil ya Sudan, mechi ya kwanza Geita ikiwa ugenini ilifungwa bao 1-0 kabla ya kushinda 2-1 kwenye mechi ya nyumbani na hivyo kutolewa kwa bao la ugenini.
