Na mwandishi wetu
Mabao ya Kennedy Musonda na Fiston Mayele, leo Jumapili yameiwezesha Yanga kutoka na ushindi wa 2-0 dhidi ya US Monastir ya Tunisia na kufuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga inakuwa timu ya pili ya Tanzania kufuzu hatua hiyo katika mashindano ya klabu Afrika baada ya Simba nao kufuzu hatua kama hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika takriban saa 24 zilizopita.
Musonda aliipatia Yanga bao la kwanza katika dakika ya 33 akiitumia vizuri krosi iliyochongwa na Jesus Moloko na kuifanya timu hiyo iende mapumziko ikiwa mbele.
Dakika 14 baada ya kuanza kipindi cha pili, Mayele aliwainua kwenye viti mashabiki wa Yanga alipoandika bao la pili akiitumia pasi ya Musonda.
Ushindi huo mbali na kuiwezesha Yanga kufuzu robo fainali pia unaifanya timu hiyo kuongoza Kundi D licha ya kuwa sawa kwa pointi na US Monastir, (pointi 10) Yanga inaneemeka na wastani mzuri wa mabao.
Katika mechi nyingine ya Kundi D iliyochezwa leo, mambo hayakuwa mazuri kwa TP Mazembe ya DR Congo ambayo ikiwa ugenini nchini Mali ilichapwa na Real Bamako mabao 2-1.
Matokeo hayo yanaifanya Mazembe kuburuza mkia katika kundi hilo ikiwa na pointi tatu wakati Real Bamako inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tano.
Kimataifa Yanga yatua robo fainali
Yanga yatua robo fainali
Read also