Na mwandishi wetu
Kiungo wa Singida Big Stars, Bruno Gomes amekana fununu za kuwaniwa na Yanga, akisema anachotaka kwa sasa ni kuisaidia timu yake kumaliza Ligi Kuu NBC nafasi za juu ili kuacha historia itakayomfanya akumbukwe.
Bruno amekuwa akihusishwa kuhitajika Yanga na anatajwa huenda msimu ujao akajiunga nao katika dirisha kubwa la usajili.
Mchezaji huyo raia wa Brazil alisema anatamani kuiona timu yake inapata mafanikio na hasa kumaliza nafasi nne za juu na kwamba tetesi juu yake kwamba amefuatwa na Yanga si za kweli.
“Hakuna timu yoyote ligi kuu iliyonifuata kutaka huduma yangu, ninachotamani kwa sasa ni kufanya kazi kwa bidii na kuisaidia Singida kuwa katika nafasi ya juu kwenye ligi na kulikuza jina la Singida Big Stars.
“Malengo yangu ni kufanya kazi kwa bidii na kuisaidia Singida kuwa kileleni na kusaidia jina la timu kukua kwa kuvaa hii jezi ya Singida, natamani kukumbukwa popote niendapo kwa huduma nitakayotoa nikiwa hapa (Singida),” alisema Gomes.
Bruno amekuwa akifanya vizuri kwa sasa, kiasi cha kutajwa kuwakuna mabosi wa Yanga na kuhitaji huduma yake msimu ujao.
Licha ya kucheza nafasi ya kiungo, amefanikiwa kufunga mabao tisa hadi sasa kwenye ligi, nyuma ya kinara Fiston Mayele wa Yanga aliyefunga mabao 15 na Saido Ntibazonkiza na Moses Phiri wa Simba waliofunga mabao 10 kila mmoja.
Singida BS iliyopanda kushiriki ligi kuu msimu huu imekuwa ikifanya vizuri tangu kuanza kwa msimu, ikishikilia nafasi ya tatu baada ya mechi 25, ikiwa imeshinda mechi 14, sare sita na kupoteza mitano na kujikusanyia pointi 48.
