Na mwandishi wetu
Timu ya Simba imeeleza kutambua ugumu uliopo kupambana na Ihefu kwenye michezo miwili ya karibuni lakini imeeleza kuwa watajipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi na kusonga mbele.
Simba itavaana na Ihefu itakayokuwa kwao kwenye mchezo ujao wa ligi lakini pia juzi imepangwa kucheza nayo kwenye robo fainali ya Kombe la FA (ASFC).
Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally ameeleza kuwa wanafahamu namna gani mambo yalivyo magumu mbele ya Ihefu lakini wanasuka mipango ya kuhakikisha wanapata ushindi kwenye Kombe la FA na kusonga mbele kulekea kuchukua ubingwa huo.
“Tunakutana mara mbili sasa, kwenye Kombe la FA pia mechi itakuwa ngumu kutokana na uimara walionao Ihefu sasa, usajili walioufanya ni mzuri lakini inafahamika sisi tunataka ushindi, lengo letu kuchukua ubingwa huu.
“Hivyo lazima tupambane, lazima tuwe na mikakati juu ya hili kuhakikisha tunashinda hapa na tunasonga mbele kuelekea kutwaa ubingwa huu, hakika tunauhitaji ubingwa wa FA na Ihefu ni miongoni mwa timu unazokutana nazo kwenye hatua kama hii hivyo tutapambana zaidi,” alisema Ally.
Katika droo hiyo, mshindi wa Simba na Ihefu atakutana na mshindi wa Mtibwa Sugar dhidi ya Azam FC. Kwenye robo nyingine itazikutanisha Yanga dhidi ya Geita Gold na mshindi atapepetana na mshindi wa mechi ya Singida Big Stars dhidi ya Mbeya City.
Nusu fainali ya kwanza ya michuano hiyo itapigwa Uwanja wa Nangwanda, Mtwara wakati nusu fainali ya pili itachezwa Uwanja wa Liti, Singida na fainali itakuwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Soka Simba wanaijua vizuri Ihefu
Simba wanaijua vizuri Ihefu
Read also
