Na mwandishi wetu
Mabondia mahasimu, Iddy Pialali na Mfaume Mfaume leo Jumatano wamesaini mkataba wa kurudiwa kwa pambano lao linalotarajiwa kufanyika Septemba Mosi, mwaka huu.
Hafla ya utiaji saini wa pambano hilo ilifanyika kwenye viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam huku kila mmoja akitamba kumaliza pambano mapema.
Pambano hilo lililopewa jina la King Of The Night linaloteka hisia za wengi kutokana na upinzani uliopo baina yao na kambi zao, linarudiwa baada ya lile la awali lililopigwa Arusha kuvunjika.
Pambano hilo la raundi 10 lililopigwa Desemba 26 mwaka jana lilivunjika raundi ya kwanza tu baada ya kutafsiriwa kuwa mabondia hao waligongana vichwa vilivyopelekea Pialali kupasuka usoni.
Hata hivyo mara baada ya kuingia mkataba huo, Mfaume alitamba kuwa atahakikisha anamchakaza mpinzani wake na kama haitakuwa hivyo basi ataacha mchezo wa ngumi.
“Tusiangalie yaliyopita ilikuwaje, Watanzania wote waliona kilichotokea, hakuna kichwa ni uoga tu, sasa siku hiyo kukimbia hakuna. Mama Mfaume amesema mwanangu ‘kaza buti’.
“Tangu niko mdogo, mama yangu ananiambia hivyo, maana yake pambana, fanya mazoezi kwa bidii halafu kasema raundi ya tatu mwisho, Bi Mkubwa nimenukuu kauli yako, huyu asipoamkia ICU (chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum), naacha boxing. Mama Mfaume kaongea na timu yangu timu ya Mabibo siongei sana, nasemaje tupigane mpaka mmoja afe,” alisema Mfaume.
Naye Pialali alisema: “Mapepe, muoga anatetemeka tetemeka, mwanaume anaongea sana? Mwanaume haongei sana. Nasema niko, safi niko salama, Mfaume safari hii kazi anayo.
“Huyu (Mfaume) ni kondoo sio bondia sasa huyu kondoo dawa yake nishaipata tayari, kuna watu anawategemea lakini huyu kondoo nampiga ‘knockout’ mbaya sababu sio bondia, hamalizi huyu hana maajabu.
“Mfaume kampiga nani hapa Tanzania? Sisi tunacheza ngumi hatuogopi, kazi anayo, Manzese msiwe na presha, hapa anajikaza tu ila tutampiga,” alitamba Pialali.
