Na mwandishi wetu
Kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama amechaguliwa kwenye kikosi cha wiki cha mechi ya nne ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na beki wa timu hiyo, Shomari Kapombe.
Sambamba na hilo, kiungo huyo Mzambia pia ameingia kwenye kinyang’anyiro cha mchezaji bora wa wiki wa michuano hiyo ambayo Simba inashiriki ikishika nafasi ya pili.
Mbali na Chama, beki wa kulia wa Simba, Shomari Kapombe pia amejumuishwa kwenye kikosi hicho kilichowekwa wazi na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Katika kikosi hicho Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Raja Casablanca na Wydad Casablanca za Morocco zilitoa wachezaji wawili-wawili pia huku Al Hilal ya Sudan, JS Kabilye (Algeria) na Zamalek (Misri) zikitoa mchezaji mmoja kila moja.
Kwenye mechi ya wiki hiyo, Simba ilishinda kwa bao 1-0 dhidi ya Vipers kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, bao hilo likifungwa na Chama na kuifanya Simba kukaa nafasi ya pili ya Kundi C ikiwa na pointi sita dhidi ya 12 za vinara Raja.
Katika kinyang’anyiro cha mchezaji bora wa wiki ambacho mshindi anatarajiwa kutangazwa leo, Chama alikuwa akiwania dhidi ya Walid Sabar wa Raja, Peter Shalulile wa Mamelodi na Ahmed Zizo wa Zamalek.
Chama pia amejumuishwa kwenye wachezaji watano waliofunga mabao mazuri zaidi katika wiki hiyo pamoja na Mohamed Nahiri wa Raja walipoiadhibu Horoya mabao 3-1, Marouf Tchakei (AS Vita) walipofungwa na Kablyie mabao 2-1 na Marcelo Allende na Teboho Mokoena wa Mamelodi walipoiadhibu Al Ahly mabao 5-2.
Kwenye kikosi cha wiki za mechi za tatu za michuano hiyo Simba iliwakilishwa na beki wao Henock Inonga, aliyefunga bao pekee dhidi ya Vipers walipokuwa ugenini.
Kimataifa Chama, Kapombe wapendeza CAF
Chama, Kapombe wapendeza CAF
Read also
