London, England
Kocha wa Manchester United, Erik ten Hag ameponda matumizi ya VAR katika Ligi Kuu England akidai hayaeleweki baada ya kushuhudia kiungo wake Casemiro akipewa kadi nyekundu kwa mara ya pili.
Casemiro (pichani kulia) alipewa kadi hiyo katika mechi ya jana Jumapili na Southampton iliyoisha kwa sare ya 0-0 baada ya kumchezea rafu Carlos Alcaraz na mwamuzi Anthony Taylor akaamua kutumia VAR.
Ten Hag alichukizwa na matumizi ya VAR na kutolea mfano tukio la beki wa Leicester City, Ricardo Pereira kutoadhibiwa kwa kumchezea rafu Joao Felix wa Chelsea, rafu inayofanana na ambayo Casemiro anadaiwa kumchezea Alcaraz.
Kocha huyo pia alisema timu yake ilitakiwa kupewa penalti baada ya Armel Bella-Kotchap wa Southampton kuunawa mpira wa krosi uliopigwa na Marcus Rashford katika eneo la penalti.
“Ninachokiona ni kukosekana maamuzi yanayoeleweka, wachezaji hawana tena wanachojua kuhusu sera hii, unaona wiki hii ni Leicester dhidi ya Chelsea, VAR haimuliki ya katikati ya uwanja,” alisema Ten Hag.
Hii ni mara ya pili kwa Casemiro kupewa kadi nyekundu katika mechi mbili kati ya tatu zilizopita za Ligi Kuu England baada ya kuonyeshwa kadi hiyo mara ya kwanza katika mechi dhidi ya Crystal Palace.
Katika mechi na Palace, Casemiro ambaye pia ni kiungo wa timu ya Taifa ya Brazil, picha za VAR zilimkuta na hatia kwa kumkwida kiungo wa Palace, Will Hughes.
Casemiro mwenye umri wa miaka 31 baada ya kupewa kadi hiyo alionekana mnyonge na kutoka uwanjani akilia na sasa atakosa kuiwakilisha timu yake katika mechi nne.
Matokeo ya mechi za Ligi Kuu England zilizochezwa jana Jumapili ni kama ifuatavyo… Fulham 0-3 Arsenal
Man Utd 0-0 Southampton
West Ham 1-1 Aston Villa
Newcastle 2-1 Wolves
