Madrid, Hispania
Waendesa mashitaka wa Hispania wanajiandaa kuwasilisha kesi ya rushwa dhidi ya klabu ya Barcelona na rais wa zamani wa klabu hiyo, Josep Maria Bartomeu kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa mwamuzi.
Habari zinadai kwamba Bartomeu anatuhumiwa kuidhinisha malipo kwa makamu wa rais wa zamani wa kamati ya waamuzi, Jose Maria Negreira kiasi cha Euro 1.4 milioni kati ya mwaka 2016 na 2018.
Hadi sasa uchunguzi wa waendesha mashtaka hao unamuangazia mwamuzi wa zamani, Jose Maria Enriquez ambaye ndiye anayedaiwa kupokea malipo hayo yaliyoidhinishwa na Bartomeu.
Klabu ya Barcelona au Barca pamoja na Bartomeu kwa pamoja watatakiwa kujitetea katika kesi hiyo na huenda wakajikuta wakikumbana na mkono wa sheria kutokana na fedha hizo zilizolipwa kwenye kampuni ya Negreira iitwayo, Dasnil 95 SL.
Marais wa zamani wa Barca, Joan Gaspart na Sandro Rosell pamoja na rais wa sasa wa klabu hiyo, Joan Laporta ambaye pia alikuwa kiongozi wa klabu hiyo kati ya mwaka 2003 hadi 2010 nao pia wataitwa kutoa ushahidi.
Akizungumza hivi karibuni, Laporta ambaye aliwahi kunukuliwa hapo kabla akisema kwamba malipo hayo ni kwa ajili ya taarifa ya kiufundi kuhusu waamuzi na uchezeshaji wao, alikana tuhuma hizo akidai klabu yake haijawahi kuwanunua waamuzi.
“Barca haijawahi kuwanunua au kuwashawishi waamuzi kwa namna yoyote, haikuwahi kuwapo dhamira hiyo, ukweli unakinzana na wale wanaojaribu kuja na habari tofauti,” aliongeza Laporta.
Inadaiwa kwamba Barca ilimlipa Negreira jumla ya Euro 7 milioni kati ya mwaka 2001 hadi 2018 kipindi ambacho klabu hiyo ilikuwa chini ya marais wanne kabla Bartomeu hajakata malipo hayo miaka mitano iliyopita.
Malipo yaliyozua utata na kuwa chanzo cha uchunguzi huo ni yale yaliyofanyika kati ya mwaka 2016 na 2018 baada ya kutiliwa shaka na maofisa wa ofisi ya ushuru.
Uefa au Fifa nao wana nafasi ya kuchukua hatua na tayari Shirikisho la Soka Hispania lilibainisha wiki iliyopita kwamba Uefa iliomba kupatiwa taarifa na nakala zote zinazohusu uchunguzi wa kashfa hiyo.
