Paris, Ufaransa
Mshambuliaji wa Paris Saint-Germain (PSG), Neymar Jr anatarajia kuwa nje ya uwanja kwa takriban miezi mitatu au zaidi kutokana na matatizo ya enka huku akitarajia kufanyiwa upasuaji.
Neymar ambaye hivi karibuni amekuwa akihusishwa na mipango ya kuihama PSG licha ya mwenyewe kusema hana mpango huo, kwa msimu huu wa Ligi I ameifungia timu hiyo mabao 13 na ana asisti 11.
Mchezaji huyo kwa mara ya mwisho aliiwakilisha PSG katika mechi ya ushindi dhidi ya Lille mwezi uliopita, mechi ambayo alitolewa uwanjani akiwa amebebwa baada ya kuumia na sasa atakuwa nje ya uwanja hadi mwisho wa msimu huu.
“Katika miaka ya hivi karibuni Neymar Jr amekuwa na matatizo ya hapa na pale katika enka ya mguu wa kulia,” ilieleza taarifa ya PSG.
“Baada ya kupata matatizo Februari 20, timu ya madaktari imeshauri afanyiwe upasuaji ili kuepuka tatizo kubwa zaidi, wataalam wote walioshauriwa wamethibitisha umuhimu wa kufanya hivyo,” ilifafanua taarifa hiyo.
“Inatarajiwa atakosekana miezi mitatu au minne kabla ya kuanza mazoezi,” ilieleza taarifa hiyo huku kocha wa PSG, Christophe Galtier akisema kwamba kukosekana kwa Neymar ni pigo kubwa.
“Ni mmoja wa wafungaji bora na mtoaji asisti kwenye Ligi I, kwa hiyo ni pigo kubwa, bila ya Neymar ni ama tutakua na viungo wawili na washambuliaji watatu au viungo watatu na washambuliaji wawili, hawa ni wachezaji ambao unaweza kuwategemea kwenye nafasi tofauti,” alisema Galtier.
PSG kwa sasa inashika usukani kwenye Ligi I ikiwa imeizidi Marseille inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi nane na leo Jumatano itaumana na Bayern Munich katika mechi ya hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.