Na mwandishi wetu
Simba leo Jumanne imejiweka pazuri katika kusaka tiketi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuilaza Vipers ya Uganda bao 1-0 na hivyo kushika nafasi ya pili katika Kundi C.
Katika mechi hiyo iliyopigwa jioni hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Simba ilineemeka na bao hilo pekee lililofungwa na Clatous Chota Chama au Mwamba wa Lusaka katika dakika ya 45 akiitumia pasi ya Sakho.
Chama kabla ya kufunga bao hilo aliumiliki vyema mpira na kuwazidi ujanja mabeki wa Vipers kabla ya kufumua shuti la chinichini lililompita miguuni kipa wa Vipers na kuibua shangwe kwa mashabiki wa Simba.
Matokeo hayo yanaifanya Simba kufikisha pointi sita katika kundi lake linaloongozwa na Raja Casablanca ya Morocco ambayo leo nayo imeishindilia Horoya FC ya Guinea mabao 3-1 na hivyo kufikisha pointi 12.
Kwa matokeo hayo Raja inaendelea kushika usukani lakini pia tayari imeshafuzu hatua inayofuata ikisubiri kuungana na timu nyingine kati ya Simba, Horoya yenye pointi nne au hata Vipers inayoshika mkia ikiwa na pointi moja.
Vipers kama itashinda mechi mbili zilizobaki kwa wastani mzuri wa mabao na Simba na Horoya zikapata matokeo mabaya katika mechi zilizobaki na hivyo kufikisha pointi saba.
Hiyo inaweza kuwa neema kwa timu hiyo kusonga mbele hali inayomaanisha kwamba kundi hilo bado gumu kwa timu hizo tatu.
Kimataifa Simba yajiweka pazuri Ligi ya Mabingwa
Simba yajiweka pazuri Ligi ya Mabingwa
Read also
