Liverpool, England
Kocha wa Man United, Erik ten Hag amesema ‘walipoteza mwelekeo’ katika kipigo cha mabao 7-0 mbele ya Liverpool jana Jumapili, matokeo ambayo yamemkasirisha ingawa amejipa matumaini.
Hicho ni kipigo kikubwa kwa Man United, katika mechi ambayo walimaliza dakika 45 za awali wakiwa nyuma kwa bao 1-0 lakini matumaini ya kusawazisha yalififia kadri muda ulivyokwenda kabla ya kufungwa mabao mengine sita.
“Kipindi cha pili hatukuwa sisi, hatukuwa katika kiwango chetu, hatukucheza kama timu,” alisema kocha huyo kutoka Uholanzi ambaye huu ndio msimu wake wa kwanza na timu hiyo.
Alipoulizwa kama amekasirika kwa namna timu yake ilivyocheza hasa kipindi cha pili, Ten Hag alisema, “ndio, hiyo ni wazi na nashangaa kwa sababu nimekuwa nikiiona hii timu wiki na miezi iliyopita ikiwa makini na yenye dhamira na mtazamo wa kupata ushindi.
“Hatukushikamana na mpango wetu, tulipoteza mwelekeo, hatukufanya kazi yetu, hatukuwabana kuanzia nyuma, na hilo si jambo ‘profesheno’,” alisema.
“Tumewaangusha mashabiki na hilo limenikatisha tamaa na kunikasirisha, ni lazima tujiangalie katika ukweli huo, ni ujumbe mzito ambao tunaupata, kilikuwa ni kiwango kibaya na cha ovyo cha mwaka,” alisema Ten Hag.
Ten Hag hata hivyo alijipa matumaini akikiri kukumbana na hali kama hiyo siku za nyuma na anaamini watarudi katika ubora wao akitolea mfano matokeo ambayo hayakuwa ya kuridhisha dhidi ya Brentford na Man City lakini walikaa sawa na kupata matokeo mazuri.
Mechi ijayo ya Man United itakuwa Alhamisi hii dhidi ya Real Betis katika Europa Ligi na Jumapili katika Ligi Kuu England wataivaa Southampton, timu inayohaha kujinasua na janga la kushuka daraja.
