Na Hassan Kingu
Haishangazi beki Henock Inonga Baka wa Simba kuibuka kinara wa tuzo ya mchezaji bora wa mashabiki kwa mwezi Februari, tuzo inayodhaminiwa na Kampuni ya Emirate Aluminium Profile.
Tuzo hiyo inayoandamana na kitita cha Sh milioni 2 ni ishara ya kutambua mchango wa mchezaji hapo hapo ikionyesha thamani ya mchezaji huyo kwenye timu ya Simba.
Kwa Inonga tuzo hiyo kakabidhiwa mtu sahihi kwa mwezi Februari, na jambo zuri ni kwamba ameendelea kuonyesha ubora wake hadi sasa baada ya kutwaa tuzo hiyo. Anahitaji pongezi kwa hilo.
Na kama kuna sehemu ndani ya kikosi cha Simba yenye suluhisho sahihi, la kudumu na la muda mrefu basi sehemu hiyo ni nafasi ya beki wa kati anayocheza Inonga.
Hajaanza mwezi Februari au Machi mwaka huu, tangu atue Simba misimu miwili iliyopita akitokea DC Motema Pembe ya kwao DR Congo, Inonga amekuwa akionesha kiwango kikubwa na kuwa mhimili wa nafasi ya ulinzi Simba.
Inonga ambaye mashabiki wa Simba wamempachika jina la Varane akifananishwa kiuchezaji na beki wa zamani wa Real Madrid ambaye kwa sasa anaitumikia Man United.
Inonga alianza kujizolea umaarufu baada ya kumdhibiti mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele kwenye mechi mbili za Dar Derby katika msimu wake wa kwanza akiwa Simba.
Mapema alionesha ukomavu, akili na ujasiri wa hali ya juu na kuaminiwa na Wanasimba kutokana na kipaji alichonacho.
Ufanisi wa kazi za Inonga uwanjani umeendelea kuiweka salama Simba hata baada ya msimu uliopita kuondoka kwa beki aliyekuwa tegemeo, Paschal Wawa au kupungua kwa kasi ya Erasto Nyoni.
Awali ilionekana Joash Onyango anapaswa kutafutiwa mtu wa kusaidiana naye kutokana na kazi zake nzito uwanjani lakini ujio wa Inonga umebadili taswira na sasa yeye ndiye anayetafutiwa mtu wa kumsaidia kazi zake zinazotumia akili mno.
Ingawa Mohamed Ouattara aliyesajiliwa Simba msimu huu alitua kumpa changamoto Inonga lakini uimara wake umeendelea kumbakisha kikosi cha kwanza.
Licha ya Inonga kukaba kwa akili, kupiga ‘tackling’ za kupendeza dhidi ya wapinzani lakini pia anaburudisha na kusisimua mioyo ya mashabiki anapofanya ufundi wa kufinya, kupiga chenga akiwa eneo lake la ulinzi bila wasiwasi na mambo yakaenda sawa.
Kwa kifupi bado anaweza kukuburudisha kwa kucheza kama ‘mtu wa mwisho’ na hiyo ni kutokana na faida nyingine aliyonayo ya kumudu kucheza kama kiungo mkabaji. Inonga ana faida lukuki mno!
Simba ilifanya jambo la kupongezwa baada ya Desemba, mwaka jana kutangaza kumuongezea mkataba mchezaji huyo mpaka mwaka 2025. Maana yake wameridhishwa na ulinzi unaofanywa na beki huyo na wanafurahi usalama wa lango lao likiwa chini yake.
Msimu huu Inonga ameendelea kuonesha ubora wake hasa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya wikiendi iliyopita kuifungia Simba bao pekee ikiwa ugenini Uganda dhidi ya Vipers na kuipa ushindi na bao la kwanza tangu kuanza kwa michuano hiyo msimu huu.
Ndio maana haikushangaza kumuona akiingia kwenye kikosi bora cha wiki ya tatu ya michuano hiyo pamoja na wakali wengine kama Raed Bouchniba na Mohamed Hammouda wa Esperance, Makabi Lilepo (Al Hilal), Lema Mabidi (AS Vita), Jamal Harkass (Raja), kipa wa Mamelodi Sundowns, Ronwen Williams.
Hii si mara ya kwanza Inonga kuiokoa Simba, mfano msimu huu wakati jahazi linazama dhidi ya Kagera Sugar, beki huyo aliifungia bao timu hiyo na kulazimisha sare ya ugenini ya bao 1-1.
Usisahau msimu uliopita ambao ndio ulikuwa msimu wa kwanza kwa Inonga, aliibuka beki bora wa msimu wa Ligi Kuu NBC.
Pia, msimu huo mwezi Aprili alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi wa Simba, kitu ambacho amekirudia msimu huu kwa juzi kutangazwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Februari!
Ikumbukwe tuzo hiyo kwa msimu hutolewa takriban mara nane pekee kulingana na muda ambao ligi inachezwa, hivyo ndani ya kikosi cha wachezaji 30 kuibuka mchezaji bora wa mwezi kila msimu angalau mara moja tena kwa beki, si jambo rahisi.
Inonga haimbwi sana kama Clatous Chama au ilivyokuwa kwa Luis Miquissone au Meddie Kagere lakini umuhimu wake ni mkubwa na kila kukicha anazidi kulidhihirisha hilo kwa namba anazoandika kila msimu.
Kocha wa timu ya taifa ya DR Congo, Sebastien Desabre anaufahamu ubora wa Inonga, licha ya kuwa na machaguo mengi ya mabeki lakini amemjumuisha pia beki huyo wa zamani wa FC Renaissance kwenye kikosi chake. Anatambua dhahabu inayopatikana miguuni mwa Inonga.
Itoshe kusema kwamba Inonga ni msaada mkubwa Simba, ni beki mnyumbulifu mwenye akili, anamudu kucheza nafasi zaidi ya moja na kuna wakati anacheza rafu inapobidi ili kuitetea Simba.
Simba itambue zaidi thamani yake sasa na ifahamu mapema mipango yao ya baadaye kuhusu beki huyo maana kwa timu zilizoendelea kwa mtu mwenye msaada kama huyu anapaswa kulindwa kwa vifungu vingi vyenye faida kwa Simba na mchezaji hapo baadaye.
Sifa moja kubwa ya Inonga ni ukweli kwamba kipaji chake kimeendelea kuwa hivyo hivyo kwa wakati wote, hajatetereka au kuporomoka, zaidi ameendelea kuwa mtu muhimu katika kikosi cha Simba. Tumpongeze kwa hilo.
Ndio kwanza anamalizia msimu wake wa pili tangu atue Simba japokuwa bado ana mkataba mrefu lakini lulu kama hii haipaswi kupita tu Simba ikafanya kazi zake kisha ikaondoka kwa urahisi. Ni aidha pesa ndefu au huduma ya mrefu iliyotukuka!
Makala Tumpongeze Inonga wa Simba
Tumpongeze Inonga wa Simba
Read also
