Manchester, England
Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Newcastle katika Ligi Kuu England (EPL), kocha wa Man City, Pep Guardiola amesema mechi tatu zijazo zitatoa hatma ya timu yake msimu huu.
Man City katika siku chache zijazo itaumana na Crystal Palace katika EPL na baada ya hapo itacheza na RB Leipzig katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kuivaa Burnley katika Kombe la FA.
Kwa mujibu wa Pep ambaye timu yake inapambana kuwashusha Arsenal kileleni mwa msimamo wa EPL ikiwa nafasi ya pili, mechi hizo zina umuhimu wa kipekee kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa.
“Tuna siku mbili za kupumzika kwa sababu ni muhimu kwani kabla ya mapumziko ili kupisha mechi za kimataifa, tuna mechi tatu katika mashindano matatu tofauti, tutacheza na Crystal Palace, Leipzig na Burnley,” alisema Pep.
“Mechi hizo zitatoa hatma yetu na kile tutakachofanya kwa msimu wote,” alisema Pep ambaye katika mechi na Newcastle timu yake ilinufaika na mabao yaliyofungwa na Phil Foden na Bernardo Silva.
