Na mwandishi wetu
Yanga kesho inatarajia kushuka kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuumana na Prisons katika mchezo wa Kombe la FA (ASFC) hatua ya 16 bora.
Timu hizo zinazoshiriki Ligi Kuu NBC zinakutana katika hatua hiyo zikiwa katika nafasi tofauti ambapo Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 62 wakati Prisons inashika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 22.
Mchezo huo hata hivyo unatarajiwa kuwa mkali kutokana na upinzani uliopo baina ya timu hizo kila zinapokutana kama vile zilipokutana mara ya mwisho kwenye mechi ya ligi msimu huu na Yanga kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0.
Kocha msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze (pichani juu) ameeleza kuwa wanafahamu ugumu wa mechi hiyo lakini wao kama mabingwa watetezi wa michuano hiyo wamejipanga kuhakikisha wanafanya vizuri na kusonga mbele.
“Sio mchezo mwepesi kulingana na Prisons ilivyo, lakini tumejiandaa, tumejipanga kwa ajili ya mechi hii na ukizingatia sisi ni mabingwa watetezi kwa hiyo tunahitaji kulitetea taji msimu huu na haitakuwa kazi rahisi lakini tutahakikisha tunapambana kupata matokeo hata wachezaji wanalijua hili,” alisema Kaze.
Naye Kocha Mkuu wa Prisons, Mohammed Abdallah ‘Bares’ amesema licha ya timu yao kukosa matokeo mazuri hivi karibuni lakini tayari kuna mabadiliko ndani ya kikosi hicho na wanatarajia kuonesha kitu wapate matokeo na nafasi ya kuiwakilisha nchi kupitia michuano hiyo.

“Ni mechi ambayo ni muhimu kwa timu zote, kombe ambalo linaweza kumtoa mshindi kuwakilisha nchi, nafasi ambayo hata sisi tunaitaka kama vile ambavyo Yanga wanaitaka hivyo tumejiandaa vya kutosha, tunakwenda kupambana, kuwadhibiti Yanga na kupata matokeo.
“Mapungufu ya kwenye timu tumeshaanza kuyashughulikia na vijana wanabadilika, nafikiri mipango tuliyonayo dhidi ya Yanga tunaamini itatusaidia kuwakabili Yanga kikamilifu na kupata ushindi,” alisema Bares.
Yanga ilifika hatua hiyo baada ya kufanikiwa kuitungua Rhino Rangers kwa mabao 7-0 wakati Prisons ilipenya hatua hiyo kwa ushindi wa penalti 8-7 dhidi ya Mashujaa FC baada ya sare ya 2-2 baada ya dakika 90 za muda wa kawaida.
Mechi nyingine za hatua hiyo zinazotarajiwa kupigwa kesho itazikutanisha Geita Gold dhidi ya Green Warriors na Singida Big Stars itapepetana na JKT Tanzania.
