Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Namungo FC, Denis Kitambi amesema ushindani uliopo kwa sasa kwenye ligi unampa hofu ya kushindwa kutimiza malengo yao ya kumaliza msimu ndani ya tano bora.
Namungo yenye makazi yake Ruangwa mkoani Lindi, inashika nafasi ya saba kwenye msimamo ikiwa na pointi 32 katika michezo 24 iliyocheza hadi sasa.
Akizungumza na GreenSports, kocha huyo ameeleza kuwa timu nyingi ambazo wanatarajia kucheza nazo hivi sasa ni zile zinazopambana kujinasua kutoshuka daraja, hivyo wanajikuta kutika wakati mgumu kupata ushindi.
“Hakuna kitu kigumu kama kucheza na timu zinazopambana zisishuke daraja, hii inatupasa kuwa makini vinginevyo tunaweza kushindwa kufikia kile tulichokikusudia,” alisema Kitambi.
Kocha huyo aliuzungumzia mchezo wao unaofuata dhidi ya Prisons akisema ni mchezo mgumu ingawa watakuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani na ameahidi kupambana ili kupata matokeo mazuri.
Kocha huyo pia amezungumzia uimara wa kikosi chake tangu akabidhiwe ambapo alisema mwenendo wao umekuwa mzuri ingawa anaamini msimu ujao watakuwa bora zaidi kutokana na maboresho anayotarajia kufanya.
“Nitasajili wachezaji wa nguvu kukiimarisha kikosi chetu ili tuweze kugombania ubingwa kama ilivyo kwa timu za Simba, Yanga na Azam na uwezo wa kufanya hivyo tunao,” alisema Kitambi.
