Na mwandishi wetu
Beki wa Simba, Henock Inonga na mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele ni kati ya wachezaji 11 bora wa kikosi cha wiki kwa mechi za tatu za makundi za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika.
Kikosi hicho kimetajwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kikiwa na mchezaji pekee kutoka Simba na Tanzania kwa ujumla wakati Esperance ya Tunisia ikitoa wachezaji wanne katika kikosi hicho.
Inonga amejumuishwa kutokana na kiwango alichoonesha katika mechi yao ya tatu dhidi ya Vipers ambapo alifunga bao pekee kwenye ushindi wa bao 1-0 na kuiandikia Simba ushindi wa kwanza katika kundi lake.
Katika mechi mbili za awali, Wekundu hao walifungwa bao 1-0 na Horoya ya Guinea kabla ya kubugizwa mabao 3-0 na Raja Casablanca ya Morocco.
Wachezaji wa Esperance waliotajwa ni beki Raed Bouchniba, viungo Ghalyene Chaaeli, Mohamed Romdhane na mshambuliaji Mohamed Hammouda. Wengine ni mshambuliaji wa Al Hilal, Makabi Lilepo, Lema Mabidi (AS Vita), Mustafa Karshoum (Al-Merreikh), Roger Ahlolou na Jamal Harkass (Raja) na kipa wa Mamelodi Sundowns, Ronwen Williams.
Kwa upande wa Mayele naye ametajwa kwenye kikosi bora cha mechi za tatu za Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika kikosi hicho, Asec Mimosas imetoa wachezaji wawili, Kouassi Attohoula na Aubin Kouame kama AS FAR ilivyowakilishwa na Hamza Igamane na Reda Slim, US Monastir nayo imetoa wawili; Ousmane Ouattara na kipa Bechir Said.
Wengine ni Ngweni Ndasi wa Rivers United, Zineddine Belaid wa USMA, Abdallah El-Said wa Pyramids na Emmanuel Lonota wa FC Lupopo.
Mayele ameingia kwenye kikosi hicho kutokana na ufundi aliouonesha kwenye mechi yao dhidi ya Real Bamako ambapo alifunga bao kwenye sare ya 1-1 katika mechi hiyo iliyopigwa mjini Bamako nchini Mali.
Mafanikio ya Mayele na Inonga pia yameonekana nchini mwao baada ya kuitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya DR Congo wakiwa wachezaji pekee wa nchi hiyo wanaocheza soka Tanznaia kuitwa katika kikosi hicho.
Kimataifa Mayele, Inonga wang’ara Afrika
Mayele, Inonga wang’ara Afrika
Read also
