Seoul, Korea Kusini
Chama cha Soka Korea Kusini kimemtangaza kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Marekani, Jurgen Klinsmann ameteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa hilo.
Klinsmann ambaye pia amewahi kuwa mchezaji, anachukua nafasi ya Paulo Bento aliyeng’atuka katika nafasi hiyo baada ya timu hiyo kutolewa na Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia hatua ya 16 bora.
Kazi mojawapo kubwa ya Klinsimann mwenye umri wa miaka 58 ni kuhakikisha anaiwezesha Korea Kusini kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico.
“Najua timu ya Taifa ya Korea Kusini imekuwa bora na inapata matokeo mazuri katika kipindi kirefu sasa,” alisema Klinsmann ambaye mkataba wake na timu hiyo unafikia ukomo mwaka 2026.
“Ni heshima kwangu kufuata nyayo za makocha wakubwa ambao wameiongoza Korea Kusini kuanzia Gus Hiddink, hadi Paulo Bento ambaye nachukua nafasi hii kutoka kwake,” aliongeza Klinsmann.
“Nimejiandaa kufanya kazi kubwa ya kuisaidia timu ipate mafanikio katika mashindano yajayo ya Kombe la Asia na fainali za Kombe la Dunia 2026,” alisema.
Klinsmann alistaafu soka mwaka 1998 na mwaka 2004 alikuwa kocha wa timu ya Taifa ya Ujerumani hadi mwaka 2006 na kuiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya tatu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2006 zilizofanyika nchini Ujerumani.
Pia Klinsmann aliwahi kuwa kocha wa klabu aliyotamba nayo katika soka la ushindani ya Bayern Munich msimu wa 2008-09 kabla ya kuwa kocha wa timu ya Taifa ya Marekani mwaka 2011 hadi 2016.
Mtihani wa kwanza wa Klinsmann akiwa na timu ya Korea Kusini utakuwa Machi 24 wakati timu hiyo itakapoumana na Colombia katika mechi ya kirafiki.
