Na mwandishi wetu
Baada ya Geita Gold kuchapwa mabao 2-1 na Namungo Jumapili iliyopita, timu hiyo sasa imehamishia kwa nguvu zote kwenye mchezo wao wa Kombe la FA dhidi ya Green Warriors wakihitaji ushindi.
Katika mchezo huo wa hatua ya 16 bora utakaopigwa Machi 3, mwaka huu, Geita itakuwa mwenyeji kwenye Uwanja wa Nyankumbu, Geita.
Kocha Msaidizi wa Geita, Mathias Wandiba alisema wanatambua ugumu uliopo katika mchezo huo kwa kuzingatia ubora wa wapinzani wao lakini pia azma yao ya kutaka kuvuka hatua ya robo fainali ya michuano hiyo msimu huu.
“Tunatambua ugumu uliopo, kwanza Warriors huwa inakuwa bora muda wote hata kama ipo daraja la kwanza lakini pia tutapambana nayo tukiwa hatuifahamu zaidi kiufundi, hivyo tumewekeza nguvu zetu zote huko sasa kuuvuka mtihani huo,” alisema Wandiba.
“Unajua msimu uliopita tuliishia robo fainali na safari hii tunataka kusonga mbele zaidi kwa kuvuka hatua hiyo, tutatumia faida ya uwanja wa nyumbani pia tukitegemea kila mchezaji kuwajibika kupata matokeo kwenye hatua hii yenye matokeo mawili tu, kushinda au kufungwa,” alisema Wandiba.
Msimu uliopita Geita ilifungwa hatua ya robo fainali na Yanga kwa mikwaju ya penalti 7-6 baada ya kumalizika dakika 90 za kawaida kwa sare ya bao 1-1.
