Na mwandishi wetu
Usiseme MwanaFA, sema mheshimiwa waziri. Kwa sasa ndilo jina sahihi la msanii wa muziki wa kizazi kipya, Hamis Mwinjuma ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo.
MwanaFA ametangazwa Jumapili hii kushika wadhifa huo baada ya mabadiliko ya baraza la mawaziri na viongozi kadhaa yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Msanii huyo ambaye ametamba na nyimbo kadhaa lakini zinazokumbukwa kwa miaka ya karibuni ni ‘Habari ndiyo hiyo’ na ‘Bado nipo nipo sana’, anachukua nafasi ya Pauline Gekul aliyehamishiwa wizara ya sheria na katiba.
MwanaFA ambaye ni mbunge wa jimbo la Muheza mkoani Tanga aliingia bungeni mwaka 2020 baada ya kuchuana kwenye kura za maoni na mkurugenzi wa zamani wa mashtaka, Adadi Rajab.
Na ingawa MwanaFA alishindwa kwenye kura hizo lakini jina la msanii huyo lilipitishwa na vikao vya juu vya chama chake CCM kabla ya kuchaguliwa kwa kura nyingi na wananchi wa jimbo la Muheza.
Mara baada ya uteuzi wa msanii huyo kutangazwa, maoni mbalimbali yamekuwa yakitolewa kwenye mitandao ya kijamii kwa baadhi ya watu kumpongeza, kumtakia heri wengine kuhoji na hata kukosoa.
Katika sanaa MwanaFA amefanikiwa kujipambanua kuwa miongoni mwa wasanii wanaoimba mashairi yenye ujumbe katika jamii na ambayo yamefanikiwa kuliteka soko la muziki ndani na nje ya nchi.
Mfano wa mashairi yake katika ‘Habari ndiyo hiyo’ yameendelea kuwa njia mojawapo ya kufikishiana ujumbe kwa namna tofauti katika maisha ya kawaida iwe kwa kukosoana, kusimangana au kukumbushana jambo.
Mashairi ya ‘Bado nipo nipo’ yameendelea kutumiwa katika jamii hasa kwa vijana wanaochelewa au ambao hawataki kuoa.
Nje ya hilo, MwanaFA ambaye amekuwa mjumbe wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata pia alionyesha kuwa na msimamo katika kukataa dhulma kutoka kwa mapromota ambao ilidaiwa wengi wao walikuwa wakineemeka kwa kuwadhulumu wasanii.
Msanii huyo na viongozi wengine walioteuliwa na Rais Samia wanatarajia kuapishwa rasmi Jumatatu hii jioni Ikulu mjini Dodoma.
Burudani MwanaFA sasa waziri
MwanaFA sasa waziri
Read also
