Na mwandishi wetu
Bao la dakika za nyongeza limetosha kuinyima Yanga ushindi wa pili katika mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Real Bamako ya Mali iliyoisha kwa sare ya bao 1-1.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumapili hii usiku mjini Bamako, Yanga ilitangulia kwa kupata bao katika dakika ya 58 mfungaji akiwa Fiston Mayele aliyefumua shuti la mguu wa kushoto lililojaa wavuni.
Mayele alifunga bao hilo akimalizia pasi ya Stephanie Aziz Ki ambaye kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alimuingiza dakika nane kabla ya timu kwenda mapumziko baada ya kumtoa Khalid Aucho aliyeumia.
Mfungaji wa bao la Yanga, Mayele kabla ya kuujaza mpira wavuni alimzunguka beki mmoja wa Real Bamako na kufumua shuti lililomshinda mlinda mlango wa timu hiyo.
Baada ya bao hilo, Yanga ambayo katika mechi iliyopita iliifunga TP Mazembe ya DR Congo mabao 3-1, ilionesha kila dalili za kupata ushindi wa pili katika michuano hiyo kabla mambo hayajawaharibikia.
Aliyetibua sherehe ya Yanga alikuwa ni beki wa kati wa Real Bamako, Emile Kone ambaye alikwenda juu na kuwazidi ujanja mabeki wa Yanga kabla ya kumalizia kwa kichwa mpira wa kona uliojaa wavuni.
Kwa matokeo hayo, Yanga sasa imefikisha pointi nne ikiwa nafasi ya pili kwenye Kundi D wakati US Monastir ya Tunisia ambayo imeichapa Mazembe mabao 2-0 inashika usukani na pointi zake saba.
Mazembe inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi mbili wakati Rel Bamako inashika mkia ikiwa na pointi mbili, timu zote katika kundi hilo hadi sasa zimecheza mechi tatu.
Real Bamako: Berthe Germain, Coulibaly, Traore, Djan, Kone, Coulibaly, Sidibe/Keita, Samabaly, Kamissoko/Kone, Keita na Diakite
Yanga: Diarra, Djuma Shaaban, Lomalisa, Job, Mwamnyeto, Aucho/Aziz Ki, Moloko/Farid Mussa, Bangala, Mayele, Mudathir Yahya/Mauya na Musonda/Kisinda.
Kimataifa Dakika za nyongeza zailiza Yanga
Dakika za nyongeza zailiza Yanga
Read also