Na mwandishi wetu
Licha ya Yanga kupata ushindi dhidi ya KMC, kocha Nasreddine Nabi amechukizwa na viwango ambavyo vimeoneshwa na baadhi ya wachezaji wake ambao hawapati nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza mara kwa mara.
Katika mchezo huo uliopigwa Jumatano hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikifikisha pointi 62.
Ushindi huo licha ya kuwa ni madogo lakini umeisaidia timu hiyo kuongeza pengo la pointi dhidi ya watani zao Simba hadi kufikia pointi nane kutoka tano za awali.
Nabi amebainisha kuwa mabadiliko aliyoyafanya ilikuwa ni kwa lengo la kutoa nafasi kwa wachezaji ambao hawatumiki mara kwa mara na kuwapumzisha wale ambao aliwatumia kwenye mechi za Kombe la Shirikisho Afrika ikiwemo mchezo dhidi ya TP Mazembe.
“Niombe msamaha kwa wote mliotazama mechi hii, ndio mechi mbaya kabisa tangu nianze kuifundisha Yanga kuna wachezaji wanaonekana kuridhika hawataki, kubadilika, hauwezi kuwa kwenye timu kubwa kama Yanga na akili yako haitaki kwenda mbele,” alisema Nabi.
“Halafu mchezaji asipopangwa atasema mbona anacheza yule mimi sichezi lakini ukimpa nafasi hajitumi, wachezaji wa aina hii hawana nafasi kwenye kikosi changu sababu haiingii akilini unataka kucheza Yanga ambayo ni timu kubwa lakini wewe ni mchezaji mdogo,” alisema Nabi.
Nye kocha mkuu wa KMC, Thierry Hitimana ameeleza kuwa ubora waliokuwa nao wapinzani wao Yanga na kosa lililofanywa na kipa wao David Kisu ndio limechangia wapoteze mchezo huo.
“Kwa kipindi hiki si kazi rahisi kuizuia Yanga kupata ushindi kwenye Uwanja wa Mkapa, kwa sababu ni timu inayowania ubingwa lakini pia ina ari kubwa kutokana na matokeo wanayoyapata kwenye ligi na mashindano ya kimataifa hivyo nawapongeza wachezaji wangu sababu pamoja na kupoteza mchezo lakini walipambana,” alisema Hitimana.KMC inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 23 na haijashinda mchezo wowote wa ligi tangu mwaka 2023 uanze, mechi ya mwisho kushinda ilikuwa Desemba 22, 2022 walipoifunga Prisons mabao 2-0.
