Na mwandishi wetu
Kikosi cha Simba, kimeondoka Alhamisi hii jioni kuelekea Uganda kwa mchezo wao wa tatu wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Vipers huku kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akitamba kuibuka na ushindi .
Simba inashika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Kundi C ikiwa haina pointi baada ya kupoteza mechi zake mbili za awali dhidi ya Horoya AC na vinara wa Kundi hilo Raja Casablanca.
Kocha huyo ameeleza kuwa kuelekea mchezo huo walikuwa na maandalizi tofauti lengo kubwa ni kuifunga Vipers ili kurudisha matumaini ya timu hiyo kufuzu hatua inayofuata ya robo fainali.
“Unajua hatukuwa na muda wa kujiandaa kikubwa nilichofanya ni kuwajenga wachezaji kisaikolojia, unajua tumepoteza mechi mbili mfululizo lakini hatujapata ushindi kwenye mchezo wetu wa Ligi Kuu dhidi ya Azam, hivi vyote vimewatoa kwenye ari ya upambanaji,”
“Mchezo uliopo mbele yetu ni muhimu kushinda kwa mustakabali wa malengo tuliyokuwa nayo na ukweli hatukuwa na muda wa kutosha kuelekea mchezo na Vipers ndio maana nikasema maandalizi yetu yalikuwa ni ya kurudisha saikolojia za wachezaji sawa na kuwarudishia ari ya upambanaji naamini tutapata matokeo,” alisema Robertinho.
Kocha huyo ameeleza kuwa anakwenda Uganda akijua Wanasimba wanahitaji ushindi na amejipanga kuhakikisha anashusha presha zao na kupata ushindi, kitu kizuri kwake ni kuwafahamu vizuri wapinzani wao Vipers ambao alikuwa akiwanoa kabla ya kutua kwa Wekundu hao miezi miwili iliyopita.
Wachezaji 24 ambao wamesafiri na kikosi cha Simba ni Aishi Manula, Beno Kakolanya, Ally Salum, Shomari Kapombe, Izrael Mwenda, Mohamed Hussein, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Mohammed Ouattara, Joash Onyango, Henock Inonga na Erasto Nyoni.
Wengine ni Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin,Clatous Chama, Ismail Sawadogo, Saido Ntibazonkiza, Peter Banda, Kibu Denis, Pape Sakho, John Bocco, Jean Baleke, Moses Phiri na Habibu Kyombo.
Simba itaivaa Vipers kwenye Uwanja wa St. Mary’s, Enttebe majira ya saa 1.00 jioni ikifukuzia ushindi wa kwanza wa hatua ya makundi lakini pia ushindi wa kwanza baada kuukosa katika miechi zake tatu mfululizo zilizopita.