Na mwandishi wetu
Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Ally Mayay ametoa ufafanuzi wa namna maboresho ya Uwanja wa Mkapa uliopo Dar es Salaam yatakavyokuwa baada ya kupokea maelezo kutoka Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Hiyo ni baada ya siku chache Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kueleza kuwa wapo mbioni kuufanyia ukarabati uwanja huo baada ya ujumbe wa Caf uliotua nchini wiki iliyopita kwa ajili ya ukaguzi.
Mayay amesema wakaguzi hao wameainisha maeneo yanayopaswa kufanyiwa marekebisho ya ulinzi na usalama wanapokaa viongozi wakubwa uwanjani, mabenchi ya ufundi, vifaa na eneo la upasuaji mdogo na mengineyo.
“Wakaguzi wa Caf ambao walipokelewa na Simba kutokana na ushiriki wa michuano ya Afrika ya Super League pia waliainisha mambo mengi ambayo yanapaswa kurekebishwa kwenye Uwanja wa Mkapa ili pia uwe na kiwango cha Fifa (Shirikisho la Soka Kimataifa).
“Miongoni mwa maeneo yaliyoainishwa ni pamoja na eneo la kuchezea, mabenchi wanayokaa wachezaji na makocha yanapaswa kuwa na muundo wa kisasa, hata maeneo ya timu kubadili nguo, chumba cha waamuzi, na cha maofisa wa Caf,” alisema Mayay.
Pia alisema sehemu nyingine zitakazorekebishwa ni pamoja na idara ya madawa na huduma ya kwanza, dharura ikiwemo chumba pia cha masuala ya udhibiti wa dawa za kuongeza nguvu katika michezo, viti vya mashabiki jukwaani ili kukidhi hadhi ya michuano ya Super League kwa kadri Caf imependekeza kwenye ripoti yake.
“Lakini bahati nzuri Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwenye mwaka huu wa fedha imepanga pia maboresho ya viwanja vya Mkapa na Uhuru na uzuri ripoti ya Caf imesaidia kuainisha na tutatumia mshauri wa kiufundi wa Caf ili kukutana na hivyo viwango mahsusi vinavyohitajika,” alisema Mayay.
Naye meneja wa uwanja huo, Salum Mtumbuka amekaririwa leo akifafanua kuwa baada ya kukutana na maofisa wa Caf wiki iliyopita, pia walikubaliana wakati wa marekebisho mechi zitakazotumia uwanja huo ni zile za michuano ya Caf na timu za taifa huku mechi za ligi zikihamishiwa Uwanja wa Uhuru na viwanja vingine.
Habari za ndani pia zimeeleza kuwa ukaguzi mwingine wa uwanja huo kutoka kwa maofisa hao wa Caf unatarajiwa kufanyika mwezi Mei, mwaka huu.
