Na mwandishi wetu
Klabu ya soka ya Geita Gold ya mkoani Geita rasmi imezindua mfumo wa kusajili wanachama ndani ya klabu hiyo inayofanya vizuri tangu ilipopanda kushiriki Ligi Kuu Bara misimu miwili iliyopita.
Mpango huo mpya wa timu hiyo umetangazwa rasmi na Katibu Mtendaji Mkuu wa Geita, Saimon Shija ambaye amefafanua kuwa hilo limewezekana kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo ibara ya tano.
“Licha ya kuwa klabu inamilikiwa na halmashauri kwa kiwango kikubwa lakini kikatiba pia inatoa nafasi kikamilifu kwa wanachama kuwa sehemu ya umiliki wa klabu hii,” alifafanua Shija.
Alisema kuwa mwanachama atajiunga kwa kuchangia Shilingi 3,000 kwa mwezi ambazo ni sawa na Sh 36,000 kwa mwaka, hayo yakifanyika kupitia mfumo maalum wa wanachama kwa utaratibu uliowekwa na klabu.
Pia, ilifafanuliwa kwamba baada ya mwanachama kusajiliwa atapewa kadi ya uanachama iliyo katika mtindo wa kidijiti.
Shija ameeleza kuwa klabu hiyo imekusudia kupokea wanachama wasiopungua 2,000 kwa mwaka kama sehemu ya kuimarisha timu, kuifanya kuwa klabu yenye ushindani na kuongeza nguvu ya uchumi kwa timu hiyo.