Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Mbwana Makata amesema wapo kwenye maandalizi makali ya kuhakikisha wanapata matokeo kwenye mechi yao dhidi ya Kagera Sugar ili wajinasue mkiani mwa msimamo wa ligi.
Katika mchezo huo wa mzunguko wa 24 wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kupigwa Ijumaa hii, Ruvu itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Makata alisema wanajua mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na Kagera kutokuwa na matokeo mazuri hivi karibuni licha ya kupata ushindi kwenye mechi yao ya mwisho ya ligi lakini pia wana benchi zuri, ndio maana wamekuwa kwenye maandalizi stahiki dhidi ya mtanange huo.
“Kwenye mechi yao ya mwisho Kagera ilipata ushindi na sisi tulipoteza, hivyo wao watahitaji kuendelea kushinda na sisi tutahitaji kurekebisha makosa yetu tupate matokeo, kwa hiyo unaona namna gani mchezo utakuwa mgumu.
“Hata hivyo tunaendelea kujipanga kikamilifu, kimkakati kuhakikisha tunafanya vizuri tusogee juu kwenye msimamo, tunataka kufanya vizuri zaidi kwenye mechi hizi zilizobaki, tunaamini inawezekana,” alisema Makata.
Licha ya Kagera kuwa nafasi ya sita kwa pointi 29 lakini imeshinda mechi moja katika mechi zake tano zilizopita kama ilivyo kwa Ruvu inayokamata nafasi ya 16 kwa pointi 17 baada ya timu zote kucheza michezo 23.
Timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa raundi ya kwanza msimu huu, Kagera iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
