Na mwandishi wetu
Ubora wa kikosi cha timu ya Singida Big Stars unampa matumaini kocha mkuu wa timu hiyo, Hans Pluijm (pichani) kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu NBC kwenye nafasi tatu za juu.
Timu hiyo kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 44 nyuma ya Azam walio nafasi ya nne wakiwa na pointi 43 lakini huenda ikaishusha Singida kwenye nafasi hiyo ya tatu kama itashinda au kupata sare mchezo wake wa leo Jumanne jioni dhidi ya Simba.
Pluijm, raia wa Uholanzi ameeleza kuwa mikakati yao ni kuhakikisha wanashinda mechi zao zote zilizobaki ili kutimiza lengo lao ambalo ni kumaliza nafasi ya pili au ya tatu.
“Sizungumzii ubingwa sababu kuna tofauti kubwa ya pointi kati yetu na Yanga, lakini uwezo wa kupambana na timu za Azam na Simba tunao ndio maana tunapambana kuhakikisha tunamaliza kwenye nafasi hizo mbili nyuma ya kinara,” alisema Pluijm.
Kocha huyo ameeleza kuwa mapumziko ya wiki mbili ameyatumia kuimarisha kikosi chake ikiwemo kurekebisha baadhi ya mapungufu aliyoyaona kwenye mechi zilizopita ikiwemo ile dhidi ya Simba, ambayo walifungwa mabao 3-1.
Alisema pamoja na ushindani uliopo lakini kwa ubora wa kikosi chake haoni sababu ya kutomaliza katika nafasi hizo sababu hata wachezaji wake wameonesha utayari wa kuipigania timu hiyo kumaliza msimu ndani ya tatu bora.
Februari 27, mwaka huu Singida itakuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Liti ikipapatuana na Mtibwa Sugar ambapo Pluijm ametamba kuchukua pointi zote tatu na kulipa kisasi baada ya kupoteza mchezo wao wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Mtibwa uliopigwa kwenye dimba la Manungu Complex.