Liverpool, England
Mmiliki wa klabu ya Liverpool, John Henry amesema kwa sasa hawana mpango wa kuiuza klabu hiyo licha ya hapo kabla kunukuliwa akisema kwamba alikuwa akiufanyia kazi mpango wa kuiuza klabu hiyo.
Henry ambaye ni Mmarekani, Novemba mwaka jana alisema kwamba wanaufanyia kazi mchakato wa kuiuza klabu hiyo kama tu kutakuwa na faida ya kufanya hivyo kwa klabu.
Bilionea huyo kupitia Kampuni ya Fenway Sports Group (FSG), mwaka 2010 aliinunua Liverpool kwa Pauni 300 milioni na hivi karibuni ilidaiwa kwamba anataka kuipiga bei.
Baada ya taarifa hiyo ya FSG, mwenyekiti wa Liverpool, Tom Werner alisema kwamba hakuna uharaka wowote wa kulikimbilia jambo hilo.
Kwa upande wa Henry alinukuliwa na jarida moja akisema, “najua kumekuwa na mazungumzo mengi kuhusu Liverpool, lakini ukweli ni kwamba kuna michakato tunaikamilisha.
“Je tutakuwa England maisha yetu yote? Hapana. Je tunaiuza Liverpool? Hapana. Je tunazungumza na wawekezaji? Ndio. Kuna lolote litakalotokea? Naamini linaweza kutokea lakini haitokuwa kuuza klabu.” alisema Henry.
Wakati Henry akikana kutaka kuiuza klabu hiyo, Wamarekani wenzake wanaoimiliki Manchester United Familia ya Glazer inadaiwa wanajipanga kuanza mchakato wa kutafuta tajiri wa kuinunua klabu hiyo.
Miongoni mwa majina yanayotajwa kutaka kuinunua Man United ni bilionea wa Uingereza Jim Ratcliffe na bilionea wa Qatar, Sheikh Jassim Bin Hamad Al Thani.