Na mwandishi wetu
Kocha Msaidizi Yanga, Cedric Kaze amekiri timu yake kupata upinzani mkubwa wanapoumana na KMC lakini watapambana kupata ushindi kutokana na hesabu za mbio za ubingwa zilivyo.
Yanga itaumana na KMC kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ambapo Yanga itaingia ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC kwa pointi 56 huku KMC ikiwa nafasi ya 12 kwa pointi 23.
Akizungumza leo Jumanne na waandishi wa habari jijini Dar es Sakaam, Kaze alisema siku zote mchezo wao dhidi ya KMC unakuwa na upinzani mkubwa ndio maana hata mechi yao ya mzunguko wa kwanza walipata ushindi wa bao 1-0 dakika za lala salama.
“Tunapokutana na KMC huwa tunakutana na upinzani ingawa naamini sisi tuko bora zaidi kimwili na kiakili wachezaji wote wako kwenye hali nzuri isipokuwa majeruhi wa muda mrefu Abuutwalib Mshery, Benard Morrison na Denis Nkane ndio watakaokosekana kesho.
“Kikubwa ni kuwafanya wachezaji waondoe furaha ya ushindi wa mchezo uliopita wa Kombe la Shirikisho Afrika, tumetoka kucheza michezo miwili migumu lakini imetusaidia kuwa kwenye hali nzuri ya kiwango chetu kikubwa, tunapaswa kusahau yaliyopita ili tuwe na ari ya kupambana na kuzitafuta pointi tatu dhidi ya KMC,” alisema Kaze.
Kabla ya mechi hiyo na KMC, Yanga imetoka kucheza mechi mbili mfululizo za Kombe la Shirikisho Afrika, ilifungwa ugenini Tunisia mabao 2-0 na US Monastir kabla ya juzi kwenye Uwanja wa Mkapa, kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Kocha Msaidizi wa KMC, Ahmed Ally alisema wanajua wanaenda kucheza na timu bora inayoshiriki mashindano ya kimataifa na ipo kwenye nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu NBC ingawa wamepanga kupambana kwa dakika zote 90 kutafuta matokeo.
“Tunajua tunaenda kucheza mechi ngumu, sisi tunahitaji pointi kutokana na sehemu tuliyopo na wao wanahitaji pointi ili wachukue ubingwa.
“Utakuwa mchezo mzuri na bora, tumejaribu kuangalia sisi benchi la ufundi na wachezaji mipango yetu ya kwenda kucheza na timu ambayo inataka matokeo kwenye kila mchezo lakini ni mechi yenye uhitaji kwa timu zote mbili na mwisho wa siku mwenye kikosi bora ataenda kupata matokeo,” alisema Ally.
