Na mwandishi wetu
Yanga hatimaye imerejesha furaha kwa mashabiki baada ya kuilaza TP Mazembe ya DR Congo mabao 3-1 katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ya hatua ya makundi imeifanya Yanga kushika nafasi ya pili Kundi D ikiwa na pointi tatu na mabao matatu wakati kinara wa kundi hilo, US Monastir ya Tunisia ambayo iliilaza Yanga mabao 2-0 katika mechi ya kwanza, ina pointi nne.
Mazembe inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu kama Yanga lakini imezidiwa wastani wa mabao ya kufunga wakati Real Bamako ya Mali inashika mkia ikiwa na pointi 1. Kila timu imecheza mechi mbili.
Mashabiki Yanga walianza kuona raha ya mechi hiyo dakika ya saba ya mchezo huo baada ya Kennedy Musonda kufungua ukurasa wa mabao kabla ya kutoa pasi iliyozaa bao la pili lililofungwa na Mudathir Yahya.
Mudathir alipoinasa pasi hiyo dakika ya 12 ni kama alimchungulia kipa wa Mazembe, Narcisse Nlendi kabla ya kuubetua mpira kwa umakini na kujaa wavuni, bao lililoamsha shangwe kwa mara nyingine.
Mabao hayo yalidumu kipindi chote cha kwanza lakini katika dakika ya 80, Mazembe walifanikiwa kupata bao lililotokana na mpira wa adhabu uliopigwa na Alex Ngonga na kujaa wavuni.
Wakati ikiaminika mechi ingeisha kwa matokeo hayo, Tuisilia Kisinda au Tk Master katika dakika mbili za nyongeza aliiipatia Yanga bao la tatu akiitumia vizuri pasi ya Fiston Mayele.
Kwa ushindi huo Yanga mbali na kutoka mkiani kwenye kundi lake na kuchupa hadi nafasi ya pili, pia imejihakikishia kitita cha Sh 15 milioni kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyeahidi ‘kununua’ kila bao kwa Sh 5 milioni.
Katika mechi hiyo mchezaji nyota wa Yanga, Stephane Azizi Ki alianzia benchi na kuingia baadaye akichukua nafasi ya Musonda ambaye aliumia.
Katika mabadiliko mengine, kocha Nessraddine Nabi pia aliwatoa Moloko na nafasi yake kuingia Mzize na Mudathir nafasi yake ikachukuliwa na Kisinda wakati Bangala naye alitoka na kuingia Mauya.
Kikosi kilichoanza Yanga; Diarra, Djuma Shaban, Lomalisa, Dickson Job, Mwamnyeto, Khalid Aucho, Moloko, Bangala, Mayale, Mudathir na Musonda.
Katika mechi nyingine ya Kundi D Real Bamako na US Monastir zilitoka sare ya bao 1-1.
Kimataifa Yanga yarejesha furaha
Yanga yarejesha furaha
Read also
