Na mwandishi wetu
Maofisa wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) wametua nchini kwa ajili ya kufanya ukaguzi kwa timu ya Simba kuelekea ushiriki wao wa Caf Super League itakayojumuisha timu nane.
Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally ameieleza GreenSports kuwa maofisa hao wametua usiku wa kuamkia leo na ukaguzi wao kwa klabu ya Simba utadumu kwa siku tatu kabla ya ugeni huo kuondoka kesho.
Ally alisema kuwa ujio wao ni kwa ajili ya kukagua miundombinu ya klabu, ofisi za klabu, uwanja wa mazoezi na uwanja wa mechi utakaotumika kwenye ligi hiyo inayotarajia kuanza Agosti, mwaka huu.
“Ujio wao ni wa siku tatu na kwa kuwa sisi ni miongoni mwa washiriki wa ligi hiyo wamekuja kukagua miundombinu, ofisi, viwanja na kadhalika, hiyo ni katika kuweka sawa maandalizi ya ligi yenyewe ambayo tutashiriki kikamilifu,” alisema Ally.
Simba inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika pia, imeteuliwa kushiriki mtindo huo mpya wa ligi huku timu nyingine maarufu na zenye historia kubwa ya soka Afrika zikitajwa kushiriki licha ya kuelezwa timu kama Raja Athletic, Orlando Pirates na Kaizer Chiefs hazitashiriki.
Klabu nyingine zilizotajwa kuwemo kwenye ligi hiyo ni TP Mazembe ya DR Congo, Petro de Luanda (Angola), Horoya (Guinea), Wydad AC (Morocco), Esperance de Tunis (Tunisia) na Mamelodi Sundowns.
Mchakato wa Super League ulitangazwa Agosti 8, mwaka jana na Rais wa Caf, Patrice Motsepe ambapo awali ulitangazwa kujumuisha timu 24 na bingwa atajizolea Dola za Marekani milioni 11.5 (zaidi ya Sh bilioni 25.6).