Na mwandishi wetu
Benchi la ufundi la timu ya Geita Gold lipo kwenye maandalizi kabambe kuelekea mechi yao dhidi ya Ruvu Shooting wakifahamu upinzani mkali wa mechi hiyo utakaokuwepo.
Geita inatarajia kuvaana na Ruvu keshokutwa Februari 17 ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Nyankumbu.
Kocha msaidizi wa Geita, Mathias Wandiba (pichani) alisema kuwa wanafahamu ni ngumu kiasi gani kucheza na timu iliyo mkiani kwani hupambana mno kwenye mechi hizi za mwisho za ligi ili kujinasua.
“Ukiachana pia na kuwa mkiani, lakini Ruvu si timu ndogo na itataka kuhakikisha haishuki daraja na sisi pia tunataka kupata ushindi kwa ajili ya kutoka hapa tulipo tuingie kwenye nne bora ambayo nayo kila mmoja anaitolea macho hiyo.
“Lakini pia tunahitaji ushindi wa mechi hii kwa sababu ndiyo mechi yetu ya mwisho kucheza nyumbani kabla ya kwenda kucheza mechi tatu dhidi ya Namungo, Yanga na KMC hivyo tunahitaji kujitetea kwanza kabla ya kwenda ugenini,” alisema Wandiba.
Geita itakuwa dimbani ikiwa kwenye nafasi ya tano kwa pointi zake 31 wakati Ruvu inayoshika nafasi ya 15 ikiwa na pointi 17 huku kila timu ikiwa imeshacheza mechi 22 zikisalia nane kabla ya kumalizika kwa ligi.